MKURUGENZI MKAZI WA BENKI YA DUNIA NCHINI ATEMBELEA OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU



………………………………………………………………………………………………………..
Na Veronica Kazimoto
26 Mei, 2016.
BENKI ya Dunia imeahidi
kuendelea kuisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kifedha ili iweze
kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa Takwimu Rasmi nchini.
Akizungumza leo alipotembelea
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa
nchini Ms. Bella Bird amesema kutokana na umuhimu wa takwimu katika
kupanga na kupima matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
kimaendeleo, Benki ya Dunia itaendelea kuisaidia NBS ili iendelee
kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa takwimu kwa wakati.
“Ili Ofisi ya Taifa ya Takwimu
iweze kutoa takwimu kwa wakati, inahitaji kuwekeza katika matumizi ya
technolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa takwimu, hivyo Benki ya Dunia
itaendelea kutoa msaada wa kiufundi na kifedha ili kufikia malengo
yaliyoainishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya utoaji wa takwimu rasmi
nchini”, amesema Ms. Bella Bird.
Mkurugenzi huyo Mkazi
amefafanua kuwa Benki ya Dunia inatambua umuhimu wa takwimu katika
maendeleo ya nchi zote duniani ikiwemo Tanzania katika kupanga sera na
kutekeleza miradi mbalimbali ya nchi husika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ameishukuru Benki ya
Dunia kwa misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiisaidia Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ambayo imeongeza tija katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu
rasmi nchini.
“Napenda kuchukua fursa hii
kuishukuru Benki ya Dunia kupitia ujio wako kuitembelea Ofisi ya Taifa
ya Takwimu na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na ofisi hii
ikiwa ni pamoja na ukusanyaji na utoaji wa takwimu rasmi hapa nchini,”
amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema Ofisi ya
Taifa ya Takwimu imeendelea kupanua wigo wa uzalishaji wa takwimu nchini
ikilinganishwa na karne zilizopita.
Benki ya Dunia inaisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutoa
ushauri wa kitalaam pamoja na fedha kupitia Mpango Kabambe wa Kitaifa
wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini ambapo awamu ya kwanza
itakamilika mwezi Juni, 2018.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni