TATIZO LA AJIRA LINAENDELEA KUWA CHANGAMOTO KWA VIJANA ZANZIBAR
Mkurugenzi wa Idara ya Ajira
Ameir Ali Ameir amesema tatizo la ajira nchini bado ni changamoto kubwa
kwa vijana kutokana vijana wengi kukosa sifa za kuajiriwa na baadhi yao
kuchagua kazi za kuajiriwa.
Hayo ameyasema leo katika Ukumbi
wa Kidongo chekundu wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Kuwajengea
Uwezo wa Kamati za Ajira za Wilaya za Mjini na Magharibi.
Amesema vijana ndio nguvu kazi
katika jamii hivyo wana nafasi kubwa katika kulitumika Taifa kwa
kufanya kazi lakini mtazamo wa vijana bado ni tatizo na baadhi
wamejenga tabia ya uvivu unaopelekea kuwepo kwa vijana wengi wanaomaliza
masomo wakiwa wazururaji wasio na ajira.
Mkurugenzi huyo amezitaka kamati
za ajira kujipanga vizuri kuyafuatilia matatizo yanayowakabili vijana
kupitia vigezo vyao, masheha, waajiri, mtazamo pamoja Utamaduni wao ili
kuwanusuru kujiingiza katika vikundi viovu.
“NI kazi ya kamati kupita kwa
waajiri ili kuangalia Changamoto, mafanikio attitude na Utamaduni kwa
vijana pia unaweza kufahamu matatizo ya vijana kupitia vigezo vyao pia
wazee wana nafasi gani katika kuwasaidia vijana,” alifahamisha
Mkurugenzi Ameir.
Aidha amezifahamisha kamati hizo
kutafuta taarifa yakinifu kwa vijana ili kupata kujua matatizo ya ajira
yanayowakabili na kuweza kuwasaidia na kuwaingiza katika soko la
ajira.
Ameeleza kuwa vijana wanahaki ya
kupata kazi yenye heshima inayoendana na mazingira bora ambayo
yatamjenga kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kumpatia kipato cha
kujikimu kimaisha na kuondokana na utegemezi.
Akiwasilisha Mada ya Mpango Kazi
wa Ajira kwa Vijana Afisa Ajira Kutoka Idara ya Ajira Mustafa Hassan
Makame amesema serikali imeweka mikakati mbali mbali ili kuhakikisha
inakabiliana na tatizo la ajira na kuona kwanba tatizo hilo linapungua
nchini.
“Ujasiri amali ni njia ya
kutatua tatizo la ajira kwa vijana na sio ajira za serikali peke yake
hivyo vijana wana nafasi kubwa ya kujiajiri wenyewe,” ameeleza afisa
huyo.
Nae Mtaalamu kutoka Shirika la
Kazi Duniani Edmund Mushy amesema serikali pekee haiwezi kulitatua
tatizo la ajira kwa vijana ni lazima pawepo mashirikiano na wadau
wengine ikiwemo sekta binafsi na taasisi nyngine kwani nao wana
mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.
Wakichangia mada washiriki wa
mafunzo hayo wameiomba wizara kuweka mratibu wa ajira katika Wilaya
zote atakaeshughulia masuala ya ajira ili kuondosha usumbufu uliopo
katika wilaya hizo na kamati ziweze kufanya kazi walizopangiwa kwa
ufanisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni