MHE. UMMY MWALIMU AELEZEA MIKAKATI YA SERIKALI KATIKA KUHAKIKISHA USAWA WA KIJINSIA KATIKA ELIMU
Mke
wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akisoma
hotuba yake kwa wageni waalikwa na wahitimu wakati wa Sherehe za
Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya Shule ya WAMA- Nakayama.
Kaimu Balozi wa Japan hapa nchini Bw. Hiroyuki KUBOTA akisoma hotuba yake wakati wa Sherehe za Mahafali
Wahitimu
wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya WAMA -Nakayama katika
picha ya pamoja na Mwenyekiti wa WAMA mara baada ya kumkabidhi Cheti cha
Shukrani kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu yao.
Wahitimu
wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari WAMA- Nakayama wakionyesha
maonyesho ya masomo kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu, Mwenyekiti wa
WAMA, Mama Salma Kikwete pamoja na wageni waalikwa.
Dr.
Ramadhani Dau, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya WAMA-
Nakayama akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa katika Sherehe za
mahafali ya Kidato cha sita shule ya sekondari WAMA Nakayama
…………………………………………………………………………………………………
Na Philomena Marijani, WAMA Foundation
Serikali imechukua hatua maalum
za kisera na kimipango kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia
katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia. Maelezo hayo yametolewa
na Mhe.Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto wakati wa sherehe za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya
Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama yaliyofanyika mwishoni wa wiki
katika ofisi za WAMA zilizopo Kawe, Dar es Salaam.
Mhe.Ummy Mwalimu ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika sherehe hizo amesema moja ya hatua hizo ni pamoja na
kuongeza idadi ya wasichana wanaopata elimu ya msingi ili kuwepo na
idadi sawa ya wavulana na wasichana.
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2008
serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu na mafunzo ili kukidhi
matakwa ya usawa wa kijinsia. “Baadhi ya maswala ambayo yamerekebishwa
ili kuboresha mazingira ya shule yaweze kuwa rafiki kwa wasichana ni
pamoja na kuhamasisha jamii kutoa chakula shuleni, kujenga mabweni na
vyoo kwa ajili ya wasichana na pia kuongeza idadi ya walimu. Wizara
yangu pia imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na Sheria ya
Mtoto No.21 ya mwaka 2009 ambayo inasisitiza jamii kuzingatia utoaji wa
haki za msingi kwa watoto, moja ya haki hizo ni haki ya kuendelezwa.”
Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mhe. Mwalimu aliwashauri wahitimu
wa WAMA-Nakayama wasiridhike na elimu ya kidato cha sita bali
wajiendeleze kwa kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini na hatimaye
serikali ipate viongozi wengi wanawake.
Akiongea katika sherehe za
mahafali hayo Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma
Kikwete alisema Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama ilianzishwa ili
kutoa mchango katika Juhudi za Taifa za kumkomboa mwanamke kwa
kuwapatia fursa za elimu bora ya sekondari watoto wa kike wanaotoka
katika mazingira magumu wakiwemo yatima.
“Taasisi inatambua kwamba
ili mtoto wa kike aweze kupata mafanikio katika masomo yake ni muhimu
kumjengea mazingira wezeshi ya kusomea na kuishi. Ndiyo maana tuliamua
kuwajengea shule yenye mahitaji yote ya kupata elimu bora na pia kuepuka
vishawishi mbalimbali vinavyoweza kupelekea kukatisha masomo. Alisema
Mama Kikwete.
Mama Kikwete aliwashukuru wadau
wote ambao wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali tangu kuanzishwa kwa
shule ya WAMA- Nakayama na kusema ushirikiano huo umesaidia kufanikisha
ndoto ya kuwasaidia watoto wa kike na matunda yake yanaonekana kwa
wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita.
Akisoma hotuba yake Kaimu wa
Balozi wa Japan hapa nchini,Bw. Hiroyuki KUBOTA alisema shule hii
iliweza kuanzishwa kwa msaada kutoka kwa Bw. Nakayama wa Japan ambaye
alichangia hela za ujenzi wa shule. Aliongeza kuwa Ubalozi wa Japan
hapa nchini umekuwa ukisaidia shule katika masuala mbalimbali ikiwemo
maboresho ya sick- bay, maabara, na kwa sasa ubalozi unasaidia upanuzi
wa jengo la utawala ambao utamalizika baada ya muda mfupi.
Shule ya Sekondari ya WAMA-
Nakayama iliyopo Nyamisati, Rufiji katika Mkoa wa Pwani ilianza rasmi
mwaka 2010. Shule inasaidia wasichana yatima na waliotoka katika
mazingira hatarishi kutoka mikoa yote Tanzania bara na visiwani. Jumla
ya wanafunzi wa kike 27 watamaliza kidato cha sita mwezi mei mwaka huu
katika michepuo ya ECA na PCB.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni