Waandishi Wawili Watwaa Tuzo ya Uandishi Wa Masuala ya Kodi na Ukusanyaji Mapato

Mshindi
wa pili wa tuzo ya Uandishi wa habari za Kodi na Makusanyo ya Mapato ya
Serikali mwaka 2015 Bw. Nuru Hassan (kulia) akipokea cheti kutoka kwa
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo
(kushoto) aliyemuwakilisha Kamishna Mkuu wa TRA katika sherehe
zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam tarehe
29 Aprili 2016
………………………………………………………………………………………………..
Kwa mara ya kwanza katika
historia ya Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari, ambazo hutolewa
na Baraza la Habari Tanzania (MCT), waandishi wawili wameshinda tuzo ya Uandishi wa Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali kwa mwaka 2015
Waandishi hao wawili, Valeria
Mwalongo, mwandishi wa Redio Tumaini aliyeshika nafasi ya kwanza na Bw.
Nuru Hassan kutoka Afya Redio aliyeshika nafasi ya pili katika
kinyang’anyiro hicho ni washiriki na washindi wa kwanza kupata tuzo hiyo
ambayo imeingizwa kwa mara ya kwanza kwa kazi za mwaka 2015
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi kutoka TRA Bw. Richard Kayombo alitoa tuzo hiyo kwa waandishi
hao kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA katika Ukumbi wa Mlimani City Dar
es Salaam ambako sherehe za kutunuku Zawadi zilifanyika.
Kutokana na ushindi huo Bw.
Richard Kayombo amesema TRA itatoa donge nono kwa waandishi wa habari
watakaoshiriki na kushinda katika kundi la uandishi wa habari za kodi na
ukusanyaji wa mapato. Mshindi wa kwanza wa 2015 Bi. Valeria Mwalongo
atajipatia kompyuta mpakato na wapili Bw. Nuru Hassan atajipatia simu
aina ya Samsung mbali na kupata tuzo na vyeti kutoka MCT.
“Mamlaka ya Mapato Tanzania
imedhamiria kuwajengea uwezo zaidi wanahabari kwa kuwaelimisha juu ya
masuala ya kodi kwa kushirikiana na MCT ambao wao watawajengea uwezo juu
ya uandishi bora kwaajili ya kuchochea ushindani zaidi katika kundi
hili mwaka ujao kwa kazi ambazo zitaandikwa katika mwaka huu wa 2016.”
Alisema Bw. Kayombo
MCT ilianzisha kundi la tuzo za
uandishi wa habari za kodi na ukusanyaji mapato baada ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania kuomba kundi hili liingizwe katika tuzo hizo kwa
kuzingatia kwamba waandishi na watangazaji wa habari wanaweza kushiriki
kwa kuandika masuala ambayo yataongeza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari.
Sehemu ya barua ya TRA kwa MCT
inasema, “TRA inatekeleza majukumu mbalimbali na mojawapo ni
kuihabarisha jamii kupitia vyombo mbalimbali. TRA pekee haiwezi
kufanikisha jukumu hili bila kuwashirikisha wadau ndio maana inaiomba
MCT kuanzisha kundi la tuzo ya uandishi wa masuala ya kodi”
Tuzo ya kundi la uandishi wa Kodi
na ukusanyaji mapato ya serikali ilijumuisha habari mbalimbali za
masuala ya kodi, masuala ya ukusanyaji wa kodi, umuhimu na matumizi ya
kodi hasa katika kugharimia huduma za jamii, nidhamu ya ukusanyaji na
utumiaji, mianya ya upotevu wa mapato, njia za kuongeza wigo wa kodi.
Nia ni kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa ili kukuza mapato ya
serikali
MCT ilizindua uwasilishaji wa
kazi za wanahabari tarehe 12 Februari 2016 kwa makundi 22 yaliyojumuisha
uandishi wa habari za Uchumi na Biashara, Michezo na Utamaduni,
Mazingira, Watoto, Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Utawala Bora, Jinsia,
Sayansi na Teknolojia, Afya ya Uzazi, Uandishi wa Uchunguzi, Elimu,
Utalii na Uhifadhi, walemavu, Mpiga picha bora wa magazeti, Mpiga picha
bora, Mchoraji kibonzo bora, Afya ya Uzazi kwa Vijana, Gesi, petrol,
Utafiti wa Madini pamoja na habari za kodi na ukusanyaji mapato.
TRA inatoa wito kwa waandishi
wote kujitokeza kwa wingi zaidi kuwania kinyang’anyiro hiki katika
mashindano ya mwaka ujao ili kuendelea kupaza sauti juu ya masuala
mbalimbali yahusuyo kodi na kujishindia zawadi mbalimbali zitakazotolewa
kwa kipindi hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni