Ijumaa, 27 Novemba 2015

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BANDARINI,AWAVUA GAMBA BAADHI YA MAAFISA TRA



Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)kutokana na upotevu wa makontena
349 yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 80.

 Akizungumza na viongozi wa mamlaka ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA,katika ziara ya kushtukiza leo,Waziri Mkuu amewataka Kamishna Mkuu wa TRA,Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA,Lusekelo Mwasena,wahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na na kwamba fesha hizo zinapatikana na zinarudi Serikalini.
 Akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na viongozi wa Serikali bandarini hapo,Waziri Mkuu aliwataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa forodha,Tiagi Masamaki na mkuu wa kituo cha huduma kwa
 wateja, Habibu Mponezya.
 “IGP,Ninaagiza watu hawa wakamatwe na kuisaidia polisi,hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,”alisema Waziri Mkuu.
 Watumishi wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA,Haruni Mpande,Hamisi Ali Omari(hakutaja anatoka kitengo gani)pamoja na mkuu wa kitengo cha Bandari Kavu (ICD In –Charge),Eliachi Mrema na alitaka wawe chini ya polisi lpaka uchunguzi utakapokamilika
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Katibu mkuu wa hazina,Dkt.Servacius Likwelile,kuhakikisha kuwa anapeleka wataalamu kutoka mawakala wa serikali Mtandao(e-Gvt)ili kukagua mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.
“Ninataka uchunguzi uanze mara moja pia tafuteni njia mabazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini pamoja na makontena yatafutwe na fedha zirudishwe serikalini.
 Akijibu maswali ya Waziri Mkuu,Kamishna Mkuu wa TRA,Rished Bade alikiri kuwepo kwa upotevu wa makontena na kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia ya wizi .
“Hata hivyo tulipoendelea na ukaguzi namba iliongezeka na kufikia 327.tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na TAKUKURU hata hivyo mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini sh.bilioni 12.6 na mpaka sasa ameshalipa sh.bilioni2.4,”alifafanua Bade.
Lakini alipoulizwa kuwa ana majina ya watumishi wanaohusika katika wizi huo hakutoa jibu la moja kwa moja na badala yake alisema anayo na ampe muda wa kuyatafuta ambapo Waziri mkuu aliyatoa na akamuonyesha orodha ya makontena yaliyopotea moaka namba za magari ambayo yalitumika kuyabebea hivyo hakuwa na jinsi na kukiri kuwa ni ya kweli.

 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi kutoka TRA na TPA.
 Hapa akionyesha orodha ya makontena yaliyopotea wakati alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini.
Waziri mkuu Majaliwa Kassim akiagana na baadhi ya viongozi kutoka TRA na TPA mara baada ya mkutano.

Maoni 1 :