WAZIRI MKUU AITAKA WIZARA KUWEKA MIKAKATI YA KUENDELEZA UVUVI KATIKA KINA KIREFU CHA BAHARI

Aidha, amezitaka halmashauri zote
nchini ziweke mikakati na mipango ya kuifanya mito na maziwa mbalimbali
nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli za
wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya
sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa
Mwalimu J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema
bado nchi haijaweza kutumia rasilimali hiyo kikamilifu.
Amesema halmashauri zinatakiwa
zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha miradi ya kufuga samaki
katika maeneo yao na wewezeshwe kupata teknolojia ya ufugaji huo.
Akizungumzia vikundi vya
wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa alishauri
waelimishwe kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana bora za
kisasa za uvuvi ili shughuli zao ziwe na tija.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amesema wakulima wanatakiwa kuzingatia matumizi ya kanuni bora za
kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu
vilivyopendekezwa na wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo
kuelekea kilimo cha biashara.
Akizungumzia kuhusu suala la
usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali alipata fursa
ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi
katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.
Amesema amefurahi kuona wakulima,
wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo wana
ari kubwa ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo
ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi kujitosheleza
kwa chakula na kuendeleza uchumi wa viwanda.
“Naamini kuwa pamoja na lengo la
kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi wataongeza ari
ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika
kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,”
alisema.
Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu
aliziagiza halmashauri zote kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa
viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa
kushirikisha taasisi za umma na binafsi, mashirika na vikundi vya
ujasiriamali katika maeneo yao.
Akizungumzia namna Serikali
ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na
wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa
katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo
michache watatengewa maeneo katika vijiji.
Awali Waziri Mkuu alitembelea
baadhi ya mabanda na maeneo ya vipando vya mazao mbali mbali yaliyoko
katika viwanja hivyo ambapo alisema ameridhishwa na juhudi zilizofanyika
katika maandalizi ya maonesho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na
uendelezaji wa uwanja huo.
“Napenda kutoa pongezi za dhati
kwa kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za kufanyia maonesho. Aidha,
natoa shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu, Mashirika yetu ya Umma na
binafsi; na watu binafsi ambao wamejenga na wanaendelea kujenga majengo
mazuri na ya kudumu,” alisema.
Pia alizindua jengo la
Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na kusema kuwa uboreshaji wa viwanja
hivyo unaonesha jinsi wadau wote katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi
na ushirika wanavyotambua umuhimu wa maonesho hayo kama njia ya kuongeza
maarifa na kumuenzi mkulima, mfugaji na mvuvi kwa kutambua mchango wao
katika uchumi wa Taifa.
Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa
mwaka huu ni kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo: vijana
shiriki kikamilifu (“HAPA KAZI TU”)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni