WAZIRI MKUU: SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KTK UJENZI WA UCHUMI

*Shinzo Abe aahidi $ bilioni 10 kwa miaka mitatu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema mabadiliko ya mifumo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hayawezi
kuletwa na Serikali peke yake bali ni lazima yahusishe pia wadau kutoka
sekta binafsi.
“Tunahitaji kushirikiana na sekta
binafsi ili tuweze kufanikisha ajenda zetu za maendeleo ziwe za kitaifa,
kikanda au za bara zima la Afrika. Ushirikiano huu utasaidia kuleta
mabadiliko dhahiri ya kiuchumi na kukuza ustawi wa jamii zetu,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi,
Agosti 27, 2016) wakati akichangia mjadala kuhusu TICAD na umuhimu wake
kwa maendeleo ya Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI)
uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta
(JICC) jijini Nairobi, Kenya.
“Wakati Serikali zinaweka
mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji, jukumu kubwa la
sekta binafsi ni kuleta mageuzi ya kiuchumi na kujenga uchumi wa viwanda
ambao ndio tunakusudia kuufikia,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria
mkutano huo wa siku mbili kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli,
alisema Tanzania inawakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka Japan
waje kujenga viwanda vya kusindika gesi asilia, kutengeneza mbolea na
kemikali mbalimbali, vyuma, nguo, bidhaa za ngozi na usindikaji wa
mazao.
Alisema ili kufikia uchumi wa
viwanda na maendeleo endelevu, ni lazima nchi za Afrika na wabia wa
TICAD wawekeze kwa pamoja na washirikiane kujenga uwezo wa rasilimali
watu, kwa kuwa ndio nguzo muhimu ya kuleta ushindani wenye tija katika
sekta ya viwanda.
Akizungumzia mpango wa mafunzo kwa
vijana wa Kiafrika katika masuala ya biashara (African Business
Education Initiative for Youth–ABE), Waziri Mkuu alisema: “Huwezi
kuzungumzia mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa viwanda bila kujenga uwezo
wa watu wetu ambao hasa ndiyo watekelezaji wa mabadiliko hayo. Ni lazima
pia tuangalie vipaumbele vya kidemografia kama kweli tunataka kukuza
uchumi kwa kujenga tabaka la watu wenye ujuzi.”
Mapema, Waziri Mkuu wa Japan,
Bw. Shinzo Abe aliwaahidi viongozi wa nchi za Afrika waliohudhuria
mkutano huo kwamba nchi yake itatoa kiasi cha dola za marekani bilioni
10 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu
barani humo.
“Ahadi hii ina nia ya kuendeleza
miundombinu ya barabara, bandari na nishati jadidifu hasa ya nishati ya
jotoardhi kwani bara hili lina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati hiyo
kwa wingi,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano
wa TICAD kufanyika barani Afrika tangu mikutano hii ianze mwaka 1993.
Mkutano huo, unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka bara la
Afrika na Japan.
Mkutano huo uliofunguliwa kwa
pamoja na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo
Abe, umehudhuriwa na marais 34 kutoka nchi za Afrika, Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-Moon na Marais wa Benki ya Dunia na Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni