Jumatatu, 1 Agosti 2016

Mgodi wa Buzwagi Wakabidhi Madawati 4494 Yenye Thamani ya Shilingi Milioni 548 Kwa Ajili ya Shule za Mkoa wa Shinyanga

Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia kupitia Mgodi wake wa Buzwagi umekabidhi madawati 4494 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 548 kwa ajili ya shule za sekondari na msingi za mkoa wa Shinyanga.Mwandishi wetu Kadama Malunde,anaripoti.
Akikabidhi madawati hayo,meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo amesema Kampuni yake imekabidhi kiasi hicho cha madawati kwa lengo la kuunga mkono jitihada za mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupunguza uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari.
“Mgodi wa Buzwagi unaunga mkono jitihada zinazofanywa na rais wa awamu ya tano,Dkt. John Pombe Magufuli katika kumaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini,tumeamua kutekeleza kwa vitendo jitihada hizo” ,alieleza Mwaipopo.
Akipokea madawati hayo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bi Zainab Telack ameupongeza mgodi wa Buzwagi kwa mchango wao uliolenga kuunga mkono jitihada za mheshimiwa rais Magufuli, katika kuhakikisha kuwa watoto wote wanakaa kwenye madawati.
“Nimefarijika sana kuona mnaunga mkono serikali,tulikuwa na upungufu wa madawati lakini kwa msaada huu wa madawati mmesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo”,alisema Telack.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote katika mkoa wa Shinyanga kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi wote wanaowaachisha masomo wanafunzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Kahama Abeli Shija akishukuru kwa niaba ya halmashauri za mkoa wa Shinyanga, ameupongeza Mgodi wa Buzwagi kwa jitihada zao mbalimbali katika kutekeleza miradi ya kimaendeleo katika mkoa wa Shinyanga na hususani wilaya ya Kahama.
Hafla hiyo ya kukabidhi madawati ilifanyika Julai 28,2016 katika Shule ya Msingi Majengo iliyoko wilayani Kahama katika halmashauri ya mji wa Kahama ambapo ilihudhuriwa pia na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga,viongozi wa wilaya ya Kahama,uongozi wa Mgodi wa Buzwagi, walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Majengo.
Continue reading →

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni