Mkurugenzi Kinondoni amewataka walipa kodi na ushuru kupewa stakabadhi za kielektroniki
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni amewataka walipa kodi na ushuru katika Manispaa hiyo kudai
stakabadhi za kielektroniki baada ya kufanya malipo ili kuziba mianya ya
upotevu wa mapato.
Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar
es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli alipokuwa
akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya njia wanazozitumia katika
ukusanyaji wa ushuru wa Manispaa hiyo.
“Napenda kuwasisitiza wananchi
kuwa unapofanya malipo yoyote ya Manispaa lazima uhakikishe unapewa
stakabadhi ya kielekroniki na iwapo hutopewa, unaruhusiwa kutoa taarifa
kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi kwenda 0767643460 na utapatiwa maelekezo ya nini cha kufanya”,alisema Kagurumjuli.
Kagurumjuli ameongeza kuwa Ofisa
yeyote atakayekaidi kutoa stakabadhi hizo atachukuliwa hatua kali za
kisheria kwani kukwepa kulipa mapato ni kurudisha nyuma uchumi wa nchi.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameyataja
maeneo ambayo mwananchi anaweza kulipia kodi au ushuru na kupata
stakabadhi za kielekroniki ni Ofisi za Manispaa, Ofisi za Kata, Benki ya
CRDB pamoja na watumishi wa Manispaa waliopo katika shughuli maalumu za
ufuatiliaji wa kodi na ushuru.
Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni ilianza kutumia mfumo wa kulipa kodi na ushuru kwa njia ya
kielekroniki mnamo mwaka 2013 , na mwaka 2015 ilipata tuzo ya ukusanyaji
bora wa mapato kwa njia hiyo kwa Tanzania na Afrika nzima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni