TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. WAZIRI UMMY MWALIMU

Takwimu zinaonyesha kuwa, hadi
kufikia tarehe 1 Mei 2016, jumla ya wagonjwa 21,124 wametolewa taarifa
na kati ya hao 331 wamepoteza maisha. Ni mikoa ya Njombe na Ruvuma tu
ambayo haijaripoti mgonjwa yeyote wa Kipindupindu tangu mlipuko huu
uanze mnamo mwezi Agosti mwaka 2015.
Ninapenda kusema kuwa, hivi sasa
kuna mabadiliko chanya katika mwenendo wa Kipindupindu, ambapo ugonjwa
huu sasa unapungua katika maeneo mengi nchini, jambo ambalo linatia moyo
sana. Takwimu za mwezi wa Aprili 2016 zinaonyesha kuwa kulikuwa na
wagonjwa 1,037, idadi ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 65 kutoka
wagonjwa 2,953 walioripotiwa mwezi Machi 2016. Katika mwezi huu wa
Aprili 2016, idadi ya wagonjwa imekuwa ikipungua kila wiki kutoka 368
wiki ya kwanza, 212 wiki ya pili, 143 wiki ya tatu hadi 104 wiki ya nne.
Mikoa iliyoongoza kuwa na
wagonjwa wapya wengi zaidi mwezi Aprili ni Mara (270), Kilimanjaro
(198), Morogoro (188) na Dar-es-Salaam (90). Idadi ya vifo
vilivyoripotiwa mwezi Aprili ni 16, wakati vifo vilivyoripotiwa mwezi
Machi vilikuwa 47. Idadi hii ya vifo ni pungufu kutoka asilimia 1.6 ya
waliougua mwezi Machi hadi asilimia 1.5 ya waliougua mwezi Aprili.
Licha ya kuwa na mwenendo chanya
katika kasi ya kupungua kwa ugonjwa huu, bado kuna mikoa inayohitaji
kuongeza juhudi zaidi katika mapambano haya. Mikoa hii ni Morogoro,
Kilimanjaro, Mara, Pwani na Dar-es-Salaam, ambapo ugonjwa huu umedumu
kwa muda mrefu zaidi. Katika mikoa hii, tutaendelea ku
peleka timu kutoka ngazi ya Taifa
kwa ajili ya kushirikiana na timu zilizopo mkoani na wilayani ili
kuongeza nguvu zaidi katika kukabiliana na tatizo hili.
Wizara ninapenda kutoa pongezi
kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
Hata hivyo, ninaendelea kusisitiza kuwa, pamoja na kuwa takwimu
zinaonyesha ugonjwa kuendelea kupungua, bado hali si salama.
Hali ya hewa iliyopo sasa katika
maeneo mengi nchini inasababisha tuwe na wasiwasi zaidi, kwani mvua za
masika pamoja na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa watu kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za usafiri na za biashara, bado ni tishio katika
kusambaa au kuibuka upya kwa ugonjwa.
Kwa kuwa hakuna mkoa wowote
ambao upo salama katika kuibuka upya kwa ugonjwa huu, bado Wizara
inaendelea kusisitiza kuwa hatua za tahadhari ziendelee kuchukuliwa ili
kuzuia maambukizi, na pia taarifa za ugonjwa ziendelee kutolewa kila
siku, hata kama hakuna mgonjwa yeyote.
Wizara yangu inatoa onyo kali kwa
Wasimamizi wa huduma za Afya Mikoani na katika Halmashauri, ambao
wanaficha taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu. Yeyote atakayebainika
kuwa anaficha taarifa hizi atachukuliwa hatua kali. Wizara yangu
inasisitiza kuwa, juhudi za kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za
udhibiti wa mlipuko huu ziendelee.
Katika kipindi hiki ambapo
ugonjwa unaendelea kupungua, Wasimamizi wa huduma za Afya Mikoani na
katika Halmashauri, waendelee kufuatilia na kuchunguza kwa kina, taarifa
zote za vifo vinavyotokana na mgonjwa mwenye dalili za Kipindupindu
kama kuharisha na kutapika. Taarifa hizi zinahitajika ili hatua
madhubuti za kuzuia vifo ziweze kuchukuliwa.
Wizara inasisitiza kwamba kila
jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya
Watanzania inatumia maji safi na salama. Ninaendelea kutoa rai kwa
wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira.
Katika kipindi hiki cha mvua za
masika, utiririshaji ovyo wa maji taka ni marufuku, na mamlaka husika
katika ngazi za vitongoji, vijiji, kata na tarafa zichukue hatua za
kisheria kwa wale wote watakaobainika kufanya jambo hili
Tunaendelea kuisihi jamii
kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia
yafuatayo:
- Utoaji na upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara, na bila kuingiliwa na viongozi wa kisiasa au kiserikali.
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu,
- Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote nchini,
- Kuhakikisha upatikanaji wa ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu.
- Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
- Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa,
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindu pindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu,
- Kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya ORS katika maeneo mbali mbali nchini ili kupunguza athari za ugonjwa
Wizara yangu pia inatoa taarifa
kwa umma kuhusu ugonjwa ambao bado haujatambulika ulioripotiwa tarehe 23
Aprili katika mkoa wa Kigoma. Hadi kufikia tarehe 29 Aprili 2016, Jumla
ya Wagonjwa 1467 wenye dalili za homa, kuumwa kichwa, kulegea mwili,
maumivu ya viungo, maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika na kizunguzungu
walipatikana katika vijiji vya Songambele, Buhigwe na Mulele katika
halmashauri ya wilaya ya Buhigwe.
Hadi sasa kijiji cha Songambele
ndicho kimeripoti wagonjwa wengi zaidi (asilimia 68%). Matibabu
yanaendelea kufanyika kwa wagonjwa wote na hakuna kifo kilichoripotiwa
hadi sasa. Uchunguzi bado unaendelea kufanyika na timu ya wataalam wa
kufuatilia mlipuko huu imeshaenda mkoani Kigoma kwa ajili ya
ufuatiliaji. Wizara yangu itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu
mwenendo wa mlipuko huu.
Wizara inawapongeza na
kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa
na katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara ili
kuutokomeza ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja na wataalamu wa sekta
mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri
pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni