REA yawezesha Wananchi kuanzisha miradi ya kiuchumi vijijini.
USAMBAZAJI
wa nishati ya umeme unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
umewezesha Wananchi wengi walioko vijijini kuanzisha miradi mbalimbali
ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu
wa Mkurugenzi Mkuu wa REA nchini Dkt. Lutengano Mwakahesya, nishati bora
inachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa jambo ambalo linasaidia kuboresha
hali ya maisha ya Wananchi wengi walio vijijini. Kwa kutambua umuhimu
huo REA kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeweza kuibua miradi
mbalimbali ya nishati vijijini ili Wananchi waweze kufaidika nayo.
Wadau hao ni
pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Bei
za Bidhaa (EWURA), Wizara ya Nishati na Madini, Asasi zisizo za
Kiserikali (AZISE), Asasi za Kijamii (AZAKI) na Sekta binafsi. Dkt.
Mwakahesya ameainisha miradi ya nishati za umeme kuwa ni pamoja na zile
zinazotumia nguvu ya upepo, jua, maji na bayogasi.
Dkt.
Lutengano ameeleza kwamba, lengo kubwa la ushirikiano baina ya REA na
Wadau hao ni kuibua miradi mbalimbali ya nishati, kutoa ruzuku na
kuwezesha upatikanaji wa ushauri wa kitaaluma kwa waendelezaji wenye
sifa katika masuala ya kiufundi, usimamiaji, uchanganuzi wa kifedha,
ugharamiaji wa miradi na mienendo mizuri ya miradi hiyo.
Amesema, REA
inahakikisha kwamba uendelezaji wa miradi ya nishati vijijini
unazingatia utumiaji wa mazingira ili kutunza vyanzo vingine vya
nishati. Ameongeza kusema kuwa REA inaongozwa na Bodi ya Nishati
vijijini ambayo husimamia uendeshaji wa Mfuko wa Nishati vijijini (REF).
Mfuko huu unasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa miradi ya Nishati.
Serikali
kupitia mfuko wa Nishati vijijini ilifadhili miradi kabambe ya
usambazaji wa umeme vijijini awamu ya kwanza na ya pili ambayo
inatekelezwa na Wakandarasi binafsi katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Utekelezaji
wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 90 na ambapo kilometa 1600 za
msongo wa kati na kilometa 97 za msongo mdogo zimejengwa na vipoza umeme
vilifungwa na wateja wa awali 18,253 wameunganishiwa umeme.
Katika awamu
ya pili mradi ulilenga kujenga vituo 6 vya kuongeza msongo wa (umeme
11/33 KV) katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na
Tunduru, ujenzi wa njia za umeme msongo mdogo na wa kati na kufunga
mashine umba (transfomer) 3100. Mradi ulilenga kuunganisha wateja
225,000 na vijiji 2,500 pindi ukikamlika na kupeleka umeme makao makuu
ya Wilaya 13.
Mradi huu
uliweza kujenga vituo 6 vya kuongeza nguvu Kigoma Vijijini, Kasulu,
Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru.Aidha mradi ulikamilisha ujenzi wa
njia za msongo mdogo na wa kati,na wateja 61,023 walipatiwa umeme. Jumla
ya vijiji 1,162 viliunganishwa kwenye gridi.
Akielezea
juu ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizoanzishwa vijijini Dkt.
Lutengano amesema, kutokana na upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini
maisha ya Wananchi yamekuwa mazuri kutokana na kuwepo kwa shughuli za
kibiashara kama vile, mashine za kusaga na kukoboa nafaka, viwanda vya
uselemala, utengenezaji wa milango na madirisha ya chuma, uuzaji wa
vinywaji baridi n.k.
Kwa upaande
wa shuhguli za kijamii, upatikanaji wa nishati wa umeme umeboresha
huduma za hospitali, vituo vya afya na kumeongezeka kwa ari ya wanafunzi
kujisomea wakati wote na pia matumizi ya kompyuta mashuleni, Kwa sasa
wanawake wajawazito wanakwenda hoapitalini kujifungua bila kulazimika
kuchukua koroboi.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, hadi mwaka 2014
kiwango cha uunganishaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya na vijijini
ulifikia asilimia 24 na kufanya Wananchi wanaopata huduma za umeme
kufikia asilimia 36 ya Watanzania waishio bara ukilinganisha na mwaka
2005 ambapo kiwango cha uunganishaji umeme kilikuwa chini ya asilimia
10.
Raarifa hiyo
inaonesha kwamba ongezeko hilo linatokana na juhudi mbalimbali za
Serikali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati vijijini
(REA) na kupunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja na
kuhamasisha Wananchi kutumia umeme.
Jumla ya
shule za sekondari 1845, zahanati na vituo vya afya 898 na hospitali 96
zimepatiwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha,
Wakala kwa kushirikiana na TAZAMA pipeline na Mfuko wa Maendeleo wa
Mafia umewezesha utekelezaji wa miradi miwili ya kupeleka umeme katika
pampu za kusukuma maji na mafuta za TAZAMA zilizoko Kisanga (Morogoro).
Akizungumzia
mafunzo yanayofadhiliwa na Wakala kwa wananchi, Meneja wa Tathmini na
Ufuatiliaji wa REA , ndugu Vestina Rwelengera alisema kwamba ni pamoja
na kuwapatia mafunzo yote ya nishati, mfano utunzaji wa vyakula kwa
kutumia nishati ya jua, miradi ya umwagiliaji, kukausha samaki na mboga
mboga.
Alitaja
maeneo yaliyonufaika na na mafunzo hayo kuwa ni Bagamoyo, Mafia na
Somanga Fungu ambapo wananchi walipata mafunzo ya kutengeneza mkaa kwa
kutumia majani makavu. Pia Wakala kupitia mfuko wa Nishati Vijijini,
ulitoa ruzuku kwa vikundi vinavyotayarisha maandiko ya miradi ili
kuwawezesha wanavijiji kupata mikopo kutoka kwenye benki zilizokubaliana
na Mfuko huo.
Akizungumzia
miradi mingine iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ya usambazaji
wa umeme vijijini ndugu Vestina aliema kwamba ni pamoja na mradi wa
SAGCOT Cluster ambao utasambaza umeme kilometa 100 , kujenga kituo cha
kupozea umeme katika mji wa Ifakara na mradi huu utaunganisha wateja
3,000.
Miradi
mingine ni ya Andoya ( Mbinga), Tulila (Songea), Yovi (Kilosa), ambayo
imeanza uzalishaji. Miradi ya Maguta ( Kilolo), Lupali (Njombe), na
Isigula (Ludewa) ambayo imeanza kazi ya ujenzi na miradi ya Mwenga
(Mufindi) ambapo jumla ya wateja zaidi ya 4,600 wameunganishwa.
Hadi kufikia
Desemba 2015 vijiji 5,009 ambavyo ni sawa na asilimia 33 vilikuwa
vimeunganishwa na huduma za umeme na miradi inayoendelea itaunganisha
vijiji vingine vipya 1,340 na kufanya jumla ya vijiji 6,349 kupata
huduma ya umeme miradi ikikamilika.
Akizungumzia
changamoto zinazoikabili Wakala, ndugu Vestina alisema kuwa ni pamoja
na Wananchi wa vijijini kushindwa kumudu gharama za kuunganishiwa umeme,
upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha na usalama wa miundombinu
kutokana na uharibifu na vitendo vya uharibifu vinavyofanywa na
wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni