TAASISI YA TIBA YA MIFUPA, UPASUAJI WA UBONGO NA MISHIPA YA FAHAMU (MOI) YAPOKEA MILIONI 20
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa ,Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) Dk. Othman Kiloloma akizungumza wakati alipokua akipokea msaada kutoka, Taasisi
ya GSM ya Dar es Salaam baada ya kumkabidhi hundi ya mfano ya Milioni
20 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba na matibabu kwa watoto wenye
matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi ambao unajulikana kama
Hydrocephalus & Spinal Bifida. Jijini, Dar es Salaam leo (PICHA NA RAYMOND URIO)
NA MWANDISHI WETU
Taasisi ya GSM ya Dar es Salaam,
imekabidhi msaada wa fedha taslimu shilingi milioni 20, kwa Taasisi ya
Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa ajili ya kununulia vifaa
tiba na matibabu kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo
wazi ambao unajulikana kama Hydrocephalus & Spinal Bifida.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi mfano wa hundi, mwakilishi wa Kampuni ya GSM,
Shannon Kiwamba, alisema wameguswa na changamoto zinazowakabili
Watanzania ndiyo maana imeamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ya kuboresha
huduma za afya hapa nchini.
Shannon alisema, pamoja na msaada wa
fedha ambazo GSM imeipa Moi, vilevile watafadhili kambi za upasuaji
(Surgical camps) kwa watoto wenye matatizo ya vichwa kujaa maji na
mgongo wazi katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dkt Othman Kiloloma, alisema
anaishukuru GSM kwa kuguswa na hali za Watanzania hususan watoto wenye
matatizo ya vichwa kujaa maji na mgongo wazi ambao kimsingi wanahitaji
kufarijiwa.
Dkt kiloloma aliongeza, GSM imefanya uamuzi sahihi wa
kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata
huduma bora za afya kwa wakati mwafaka.
Alisema, fedha zilizotolewa
na GSM zitatumika kama ilivyoelekezwa, vilevile Moi ipo tayari kutoa
wataalamu kwenda mikoani kuwafanyia upasuaji watoto katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa ili kuwapunguzia wagonjwa adha ya kusafiri kwenda Dar es
Salaam.
Taasisi ya Moi imekuwa ikichukuwa jitihada madhubuti za
kuhakikisha Watanzania hususan watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo
wazi wanapata huduma bora pale walipo, ambapo imekuwa ikipeleka wataalam
mikoani kwa ufadhili wa wadau mbalimbali na kuwafanyia upasuaji.
Takwimu
zinaonesha hapa Tanzania watoto zaidi ya 5,000 kwa mwaka wanazaliwa na
vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo watoto 400 mpaka 500 pekee ndiyo
wanapokelewa Moi.