NA RAYMOND URIO, Dar
Mchezaji wa Yanga Fc, Juma Abdul Abdul akithibitiwa na beki wa Ndanda Fc |
KlABU ya Yanga imetinga nusu fainali katika Kombe la Shirikisho FA maarufu baada ya kuilaza 2-1 Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga walitangulia kupata bao lao dakika ya 27 kupitia kwa mshambuliaji wake, Paul Nonga aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa kulia Juma Abdul.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya kiungo na Nahodha wa Ndanda, Kiggi Makassy kumchezea faulo mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma nje kidogo ya boksi.
Katika kipindi hicho, Yanga wangeweza kuondoka na mabao zaidi kama washambuliaji wake, wangekuwa makini hususan Nonga mwenyewe na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva.
Msuva alipewa pasi nzuri kwenye njia na Kamusoko dakika ya 34, lakini akagongesha mwamba wa juu, wakati Nonga naye alipewa pasi nzuri na Mzimbabwe huyo na wakati anajivuta kupiga shuti ndani ya boksi beki wa Ndanda, Paul Ngalema akaupitia mpira na kuondosha kwenye hatari.
Kipindi cha pili, Ndanda walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 56 kupitia kwa Nahodha wake, Kiggi Makassy kwa shuti la nje ya boksi baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga.
Baada ya bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la ushindi lililofungwa na beki Kevin Patrick Yondan kwa penalti dakika ya 69, baada ya beki wa Ndanda, Paul Ngalema kumkwatua winga Simon Msuva ndani ya boksi.