Watu 14 wafariki kwa ugonjwa unaosababishwa na sumukuvu
Hussein Makame-MAELEZO
Watu 14 wamefariki dunia katika
wilaya za Chemba mkoani Dodoma na Kiteto mkoani Manyara kutokana na
ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama ‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na
sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka iliyoharibika.
Hayo yamesema na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya milipuko na magonjwa
mengine leo jijini Dar es Salaam.
“Ugonjwa uliosababishwa na sumu
kuvu (Aflatoxins) uliripotiwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni, 2016
katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma na baadaye mkoani Manyara katika
wilaya ya Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza kuwa:
“Wagonjwa walikuwa na dalili za
kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na kuwa manjano sehemu
mbalimbali za mwili ambayo inaashiria kuathirika kwa ini”
Alisema mbali na vifo hivyo, hadi
kufikia Julai 31 mwaka huu wagonjwa 54 waliripotiwa kuugua ugonjwa hu
huku wagonjwa wanne wakilazwa kutokana na kuugua.
“Hadi kufikia tarehe 31, Juni
2016 kulikuwa na wagonjwa 54 na watu 14 walipoteza maisha kutokana na
ugonjwa huo.Aidha katika wiki iliyopita aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya
kutoka wilaya ya Kondoa” alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:
“Jumla ya wagonjwa waliolazwa
wodini ni wanne kati yao mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na
watatu wapo katika Hospitali ya Kondoa”
Waziri Ummy alitaja wilaya
zilizoripoti wagonjwa hao na idadi ya wagonjwa kuwa ni wilaya ya Chemba
wagonjwa 38, Kondoa wagonjwa tisa , Kiteto wagonjwa watatu, Chamwino
wagonjwa wawili na Dodoma Manispaa mgonjwa mmoja.
“Vijiji vilivyoathirika zaidi na
ugonjwa huo ni kutoka wilaya ya Chemba ambavyo ni Kinkima, Itolwa,
Mwailanje na katika wilaya ya Kondoa ni kijijini cha Ubembeni” alisema
Waziri Ummy.
Hivyo, aliitoa hofu familia
iliyopoteza watu wanne katika kijiji cha Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo
havihusiani na uchawi au kuwekewa sumu bali ni chakula cha siku ile
kilithibitika kwamba kilikuwa na sumukuvu.
Kufuatia athari hizo Serikali
itafanya uchunguzi wa kina katika wilaya kumi za Chemba, Kondoa,
Chamwino na Kiteto na wilaya nyingine za mikoa ya Sindida, Dodoma na
Manyara zinazopakana na wilaya hizo.
Alisema uchunguzi huo unalenga
kubaini hali ya usalama wa vyakula vinavyotumiwa na jamii ili kuzuia
kuenea kwa ugonjwa huo na kuwaathiri wananchi wengi zaidi wanaoishi
katika wilaya hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Taifa wa Afya wa Wizara hiyo Dkt. Fausta Mosha alisema wizara imeandaa
vipepereshi vyenye maelekezo yanayotoa elimu juu ya kijikinga kwa
kuandaa chakula kuanzia hatua ya uvunaji shambani hadi wakati wa kula.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa
Serikali Dkt. Otilia Gowelle alisema njia bora ya kupambana na ugonjwa
huo ni kuukinga kwa kuhakikisha sumu kuvu haizalishwi kutoka kwenye
nafaka.
Akifafanua kuhusu udhibiti,
Waziri Ummy alisema wanashirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi
kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi ya uhifadhi na uandaaji wa
chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa nafaka ambazo
hazijaharibika sana.
“Njia hizi ni pamoja na kuhifadhi
nafaka zilizokauka vizuri na kuchambua nafaka zilizoharibika
(zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi kabla ya
kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika rangi”
alisema.
Waziri Ummy alisisitiza Serikali
kuendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa
sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima
sumukuvu katika damu na choo kidogo miongoni mwa taasisi za ndani ya
nchi.
Inaelezwa kuwa ugojwa
wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka
uliwahi kutokea nchini Kenya mwaka 2004 na kusababisha vifo vya zaida ya
watu 100 huku wengine 200 waliathirika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni