UGONJWA WA KIPINDUPINDU BADO UPO JIJINI DAR ES SALAAM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa
kipindupindu bado upo jijini Dar es Salaam baada ya wagonjwa wapya wanne
kugundulika katika Manispaa ya Temeke jijini hapa.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo
ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kwa waandishi
wa habari juu ya magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine nchini.
Alisema mwenendo wa ugonjwa huo
kuanzia Julai 2016 ulikuwa wa kuridhisha kwani wagonjwa walipungua hadi
kufikia 173 kwa mwezi bila kifo kutoka wagonjwa 555 walioripotiwa mwezi
Juni 2016 na vifo vya watu saba.
“Mkoa wa Morogoro ni mkoa pekee
umekuwa ukiripoti wagonjwa wa kipindupindu kwa kipindi kirefu hadi
sasa.Vilivile mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa haujaripoti wagonjwa tangu
Mei 19, 2016 ila wiki iliyopita siku ya Jumamosi waliripotiwa wagonjwa
wapya wanne katika wilaya ya Temeke” alisema Waziri Ummy.
Alisema katika kipindi cha wiki
iliyopita idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeongezeka hadi wagonjwa 41
kutoka wagonjwa 30 wa wiki iliyotangulia ingawa hakuna aliyepoteza
maisha.
“Hivyo kuna dalili za kuwepo tena
ongezeko la ugonjwa wa kipindupindu jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa
haraka sana na Wizara yangu” alisema.
Alifafanua kuwa Wizara yake
imeelekeza nguvu kubwa kuendelea kuudhibiti ugonjwa huo hapa Dar es
Salaam na huko mkoani Morogoro na inafuatilia ugonjwa wa kuharisha
katika mikoa mingine ili kubaini kama kuna mgonjwa yeyote wa
kipindupindu na kuudhibiti mapema.
Aliongeza kuwa kikosi kazi cha
Taifa kinaainisha maeneo makuu ya kuyafanyia kazi mkoani Morogoro ambapo
yatajumuisha elimu kwa jamii, uvumbuzi wa namna gani ya kupatikana maji
safi na salama na matumizi vya vyoo bora.
Mbali na kueleza mikakati hiyo,
Waziri Ummy alisisitiza mikoa na halmashauri zote nchini kuendelea kutoa
taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu ugonjwa huo ili kuweza kuudhibiti
endapo utabainika kuwepo sehemu yoyote nchini.
Alisema timu ya wataalamu kutoka
ngazi ya Taifa ilifanya tathmini mnamo Juni, 2016 na kubaini upungufu
katika utoaji taarifa katika baadhi ya mikoa na hivyo Wizara yake
inashirikiana na TAMISEMI kuhakikisha inafanyia kazi mapendekezo
yaliyotolewa.
Ugonjwa wa kipindupindu ulianza
nchini tarehe 15 Agost mwaka 2015 na hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2016
watu 22,375 wameugua na kati yao wagonjwa 345 walipoteza maisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni