Ilala yawataka wafanyabiashara kuzingatia muda wa usafi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jijini Dar es
Salaaam imewataka wafanyabiashara kuzingatia muda uliopangwa na
Serikali kwa ajili ya usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi
unaofanywa kila ifikapo siku ya jumamosi.
Muda uliowekwa kwa ajili ya zoezi hilo ni
kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi, ambapo wafanyabiashara
wote watapaswa kufungua maduka na masoko yao mara baada ya zoezi hilo
kukamilika.
Hayo yamesemwa leo na Afisa wa Manispaa hiyo,
David Langa wakati alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii kuhusu
mwitikio wa wananchi juu ya zoezi la usafi wa mazingira unaofanyika kila
jumamosi na kila mwisho wa mwezi.
“Nawaomba Wafanyabiashara wenye tabia ya
kujichelewesha ili wafike baada ya muda wa usafi pamoja na wale
wanaofungua biashara kabla ya muda uliopangwa na Serikali kuacha mara
moja kwani lengo la kubadili muda wa kufungua biashara ni kwa ajili ya
kufanya usafi” alisema Langa.
Akifafanua zaidi Langa aliwatahadharisha
wananchi wanaopenda kutupa taka hovyo kuacha mara moja kwani sheria ya
afya na sheria ya mazingira inapinga suala hilo na kwa mujibu wa sheria
hizo adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo
kisichozidi miaka 6.
Kwa mujibu wa Langa alisema kuwa, suala la
usafi sio suala la Serikali pekee bali wananchi wanatakiwa walifanye
kuwa ni sehemu ya kulinda afya zao, hivyo kila mmoja anapaswa kuzingatia
usafi kwenye maeneo yanayomzunguka.
Aidha Langa alisema kila mwananchi anapaswa
kuwa mlinzi wa mwenzie kwani zoezi la kulipishwa faini bado ni endelevu,
mtu atakaemkamata mwenzie anatupa taka atapewa shilingi elfu 20 na
aliyekamatwa atatoa faini ya shilingi elfu 70.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni