CHAMA cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimepiga marufuku ujenzi holela na kazi mbali mbali za kudumu
zinazofanyika katika shamba la Chama hicho bila ya kujali taratibu za
kisheria lililopo Kirombero katika Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Kimesema kuna baadhi ya watu
wamevamia shamba hilo na kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba pamoja na
kupanda miti ya kudumu ikiwemo minazi na miembe, na miti mingine ya
kudumu bila ya ridhaa halali ya chama hicho.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Ndg. Vuai Ali Vuai wakati akikagua eneo na mipaka ya
Shamba hilo huko Kilombero alisema CCM haitowavumilia baadhi ya watu
waliofanya uvamizi wa kujimilikisha eneo halali la chama hicho bila ya
kufuata taratibu za kisheria.
Alisema Shamba hilo ni urithi wa
Chama cha Afro- Shiraz party (ASP), ambalo lilinunuliwa na ASP mwaka
1959 kabla ya mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964 kwa ajili ya
kuwapati waafrika wazalendo maeneo ya kulima na kuishi baada ya
kubaguliwa na kufukuzwa katika mashamba ya watu wengine kwa itikadi za
kisiasa.
Vuai amefafanua kwamba hakuna
kiongozi yeyote ndani ya CCM mwenye mamlala ya kugawa mali yoyote ya
chama bali chombo chenye mamlaka hayo ni Baraza la Wadhamini la CCM ndio
linaloweza kutoa ridhaa baada ya kukaa na kujadiliana na kutoa maamuzi
na siyo vinginevyo.
Ameeleza kwamba chama hicho
kitaendelea kuruhusu shughuli za kijamii zifanyike katika eneo hilo
zikiwemo ujenzi wa nyumba za ibada, skuli na visima vya maji kwa
makubaliano na utaratibu maalum unaofaa kisheria lakini siyo kwa
shughuli binafsi.
“ Watu siku hizi wamebadilika na
matapeli ni wengi tunaweza kufanya wema wa kuwaruhusu wajenge wachache
baadae na wao wakawakaribisha wengine ama kuuza maeneo hayo jambo
linaloweza kuanzisha migogoro ya ardhi hali ambayo CCM haipo tayari
kuona kinatokea.
Lakini pia natoa wito kwa watu
wote walioanza kujenga na waliokwisha maliza ujenzi lakini hawajahamia
katika nyumba zao na wanaopanda miti ya kudumu wote wasitishe zoezi hilo
mpaka watakapopewa utaratibu mwingine.”, alisisitiza Vuai na kuongeza
kuwa kama kuna mpango wa kubadili matumizi ya eneo hilo lazima chama
kikae na kujadili kwa kina kisha kitatoa maamuzi hapo baadae.
Alitoa onyo kwa baadhi ya watu
wanaofanya vitendo vya kitapeli kwa kutumia hati bandia kwa nia ya
kujimilikisha mali za CCM na jumuiya zake kinyume na sheria na kuwataka
kuacha kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai, na pia kwa Mwana CCM ni
kosa kubwa la Kimaadili.
Aidha aliwataka viongozi na
watendaji mbali mbali wa Chama hicho nchini, kuanza utamaduni wa
kutembelea na kukagua mali zote zilizokodishwa ama kumilikishwa na
taasisi ama watu ili kubaini vitendo vya udanganyifu na kuweka mali hizo
katika hali ya usalama.
Alisema kwa busara na hekima za
CCM itaweza kuruhusu shughuli ndogo ndogo ziendelee kufanyika katika
eneo hilo zikiwemo kilimo cha mpunga, mboga mboga na mazao mengine ya
muda mfupi, na kuagia viongozi wa ngazi ya mkoa Kaskazini kwa
kushirikiana na viongozi wa chama na serikali katika shehia ya kilombero
kuratibu vizuri shughuli zote zinazofanyika katika eneo hilo.
Aliwasihi watu waliopewa dhamana
za kulinda mali za chama kuwa makini na kuepuka kujiingiza katika
vitendo vya kitapeli vinavyoweza kuhujumu mali za CCM na umma kwa
ujumla.
Kwa upande wao viongozi wa CCM
katika Shehia hiyo walisema shughuli anazotambua kufanyika katika eneo
hilo ni zile za kijamii zikiwemo skuli na misima vya maji safi pamoja
na baadhi ya watu wachache waliopewa kuishi katika eneo hilo kwa muda na
siyo ujenzi wa nyumba za kudumu.
Viongozi hao walimuahidi Naibu
wa Katibu Mkuu huyo kutekeleza maagizo yote aliyopewa ili kuepusha
migogoro ya ardhi inayoweza kutokea katika eneo hilo kwani CCM ni chama
cha amani kisichotaka wananchi waishi katika matatizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni