SERENGETI BOYS YATUA GOA, KUANZA NA MAREKANI J’PILI
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti
Boys imetua salama jijini Goa, India kwa ajili michuano maalumu ya soka
ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na
Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).
Mkuu wa msafara wa timu hiyo,
Ayoub Nyenzi amesema kwamba wamepokelewa vizuri na wenyeji India na leo
asubuhi Mei 12, 2016 wachezaji watapumzika kabla ya baadaye saa 10.00
jioni kuanza kujifua kwa mazoezi mepesi.
“Napenda kuwajulisha kuwa timu
imefika salama katika Jiji la Goa na tumepokelewa vizuri na wenyeji
wetu. Kwa muda huu wa asubuhi wachezaji watapumzika mpaka saa kumi jioni
wataanza program ya mazoezi,” amesema Nyenzi.
Kikosi hicho cha wachezaji 22,
kiko chini ya Kocha Bakari Shime na kinaundwa na makipa, Ramadhan
Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni
Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.
Mabeki wa kati ni Issa Makamba,
Nickson Job na Ally Ng’anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad
Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na
washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana
Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.
Maofisa watakaosafiri na timu hiyo
ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri
wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime,
Kocha wa Makipa Mohamed Muharami, Daktari wa timu, Shecky Mngazija na
mtunza vifaa, Edward Edward.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza
leo Mei 12, 2016 kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne,
Tanzania itafungua dimba dhidi ya Marekani kwenye Uwanja wa Tilak
Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi
ya Malysia Mei 15, mwaka huu.
Serengeti Boys watashuka dimbani
tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti
Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza
dhidi ya Malaysia Mei 21.
Fainali ya michuano hiyo itachezwa
Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi
wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.
AIFF kimeandaa mashindano ya
vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana
zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni