Kipaumbele chetu ni kuboresha reli ya TAZARA- Balozi Kijazi
Serikali imesema iko tayari
kuboresha reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA) ili
iweze kufanya kazi kwa ufanisi kwani ni jambo la msingi na itashirikiana
na nchi za Zambia na China ili kufanikisha azma hiyo.
Akizungumza leo jijini Dar es
salaam Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi wakati akizindua kikao
kazi kilicho shirikisha nchi tatu ambazo ni Tanzania, Zambia na China
kuhusu maboresho ya kiutendaji ya reli ya TAZARA.
“Kipaumbele chetu ni kuboresha
reli ya TAZARA ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi, kikao hiki kitajadili
kwa kina changamoto mbalimbali zinazoikabili reli hii, pamoja na fursa
zilizopo na namna ya kutatua changamoto hizo ili kufufua uchumi wetu
kupitia reli ya TAZARA” amesema Balozi Kijazi.
Balozi Kijazi amesema kwa muda
sasa reli hii imekua ikifanya kazi bila ufanisi kutokana na sababu
mbalimbali licha ya kuwa kiwango cha mizigo kutoka bandari ya Dar es
salaam kimeongezeka kutoka tani milioni 6 mwaka 2006 hadi kufikia tani
milioni 15 mwaka 2015, reli ya TAZARA imeshindwa kuwa na uwezo wa
kusaidia kusafirisha mizigo hiyo, ambapo mwaka kila mwaka uwezo wake
unashuka kutoka kusafirisha mizigo tani 601,229 mwaka 2005/2006 hadi
tani 87,860 kwa mawaka 2014/2015.
Vile vile, licha ya kuwa nchi za
Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeongeza uzalishaji wa
shaba bado TAZARA haikuwa na uwezo wa kuhudumia ama kusafirisha shaba
hiyo, utendaji huu wa kiwango cha chini lazima ubadilike.
Aidha, Serikali imesema ina ya
dhati ya kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, na yenye
viwanda, kwa kujua kuwa uanzishwaji mzuri wa mtandao wa miundombinu hasa
reli, barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini ni chanzo muhimu ya
kutimiza azma hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa
Baraza la Mawaziri la Zambia Dkt. Rowland Msiska amesema kuna haja kubwa
ya kuboresha reli ya TAZARA kwa kuwa reli hiyo ina msaada mkubwa
kiuchumi si tu kwa nchi za Tanzania, Zambia na China bali hata nchi za
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi za Ukanda wa
Maziwa Makuu.
Aidha, amesema kuna faida nyingi
za kuboresha reli ya TAZARA ikiwemo ya gharama nafuu. Usafirishaji
mizigo kwa njia ya reli ni wa gharama nafuu kuliko barabara kwani
inagharimu senti 5 kwa tani moja kwa umbali wa kilometa moja, huku
gharama za usafirishaji kwa barabara ikiwa ni senti 12 kwa tani moja kwa
umbali wa kilometa moja.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Wizara ya Biashara ya China, Bwana. Liu Junfeng amesema Serikali yake
itaendelea kushirikiana na nchi za Tanzania na Zambia ili kuboresha
utendaji wa reli hiyo, huku akisisitiza uhusiano wa nchi hizi tatu
umeendelea kuimarika na unazalisha fursa nyingine za ushirikiano.
Reli ya TAZARA ilijengwa mwaka
1970 hadi 1976 kwa msaada wa Jamhuri ya watu wa China kama zawadi kwa
mataifa ya Tanzania na Zambia, kwa lengo la kusaidiza kuongeza njia za
usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni