CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) YAKANUSHA UTAPELI.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimelaani vikali tabia ya baadhi ya watu wanaotumia vibaya jina la
Chama hicho kuwatapeli wananchi kutoa fedha ili wapatiwe nafasi za ajira
katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) jambo ambalo sio sahihi.
Kimewataka wafuasi wa Chama hicho
na wananchi kwa ujumla kuacha tabia ya kuwaaminisha watu kwamba CCM
inatoa nafasi mbali mbali za ajira kwani kufanya hivyo ni kuwagombanisha
viongozi na wananchi wao.
Akitoa taarifa kwa Vyombo vya
Habari, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai alisema
Chama hicho hakihusiki na utoaji wa ajira ya aina yoyote, hivyo watu
wanasambaza utapeli huo kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii lengo
lao ni kuchafua taswira njema ya chama hicho.
Akifafanua zaidi Ndugu Vuai
amesema suala la ajira katika taasisi za kiserikali na binafsi
zinazolewa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa hasa baada ya kutolewa
matangazo maalum kulinga na nafasi za ajira zilizopo na sio kutumia simu
za mkononi kuwapigia watu ili waweze kutoa fedha kwa ajili ya
kuwapatiwa ajira hizo.
“Nimepigiwa simu nyingi na baadhi
ya watu wangu wa karibu wakiniuliza juu ya taarifa za Chama kuwa kuuza
nafasi za ajira, taarifa ambazo nimezipokea kwa mshangao mkubwa kwani
ndani ya chama chetu hakuna utaratibu huo” na kuongeza kusema kwamba
“nawataka wananchi kuwa macho na makini na matapeli wanaotumia hila
tofauti kuwaadaa watu kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu”. Alisisitiza Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM
Zanzibar, alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na matapeli hao na mtu
yeyote atakayepigiwa simu na kuambiwa atoe kima chochote cha fedha kwa
lengo la kupatiwa ajira na CCM asikubali kufanya hivyo na badala yake
atoe taarifa haraka katika vyombo vya dola, ili sheria ichuke mkondo
wake.
Aliwasihi wananchi kuendelea
kuamini kwamba CCM ni Chama kilichokomaa kisiasa na uzoefu mkubwa wa
kusimamia demokrasia ya kweli, usawa, haki, utawala bora, a hivyo
hakiwezi kujihusisha na vitendo viovu kwa jamii.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM
alisisitiza kua; suala la ajira za JWTZ, Idara Maalum za SMZ na zile za
Taasisi nyengine za seriikali, zote hizo zinatolewa kwa mujibu wa sheria
na kanuni zilizowekwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW).
Alisema kuwa haiwezekani hata
kidogo Chama hicho (CCM) kitowe ajira na kuongeza kuwa taarifa hizo
zinazosambazwa na watu ni za kitapeli na zinalenga kuchafua jina la
Naibu Katibu Mkuu huyo pamoja na CCM kwa jumla.
Aliwaomba wananchi wazipuuze
taarifa hizo na wawe macho na utapeli wa aina hiyo uliozagaa Zanzibar na
maeneo mengine nchini, kwani unafanywa na wapinga maendeleo ya CCM na
Taifa kwa jumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni