Benki ya Kilimo yajipanga kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa.


Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imepanga kutumia zaidi ya shilingi bilioni 40 kusaidia
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha
mwaka 2016/17 hadi 2020/21 ambao umejikita katika kuhakikisha Tanzania
inajenga uchumi wa viwanda na kuongeza kiwango cha ajira na uzalishaji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Thomas Samkyi wakati akizungumza na waandishi
wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Bw. Semkyi alisema kuwa Benki hiyo
imeamua kusaidia utekelezaji huo ili kuwezesha upatikanaji wa
utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini na kuleta
mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha
kibiashara ambao utachangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
“ Katika kuhakikisha tunaunga
mkono Sera ya Kujenga Uchumi wa Viwanda nchini Benki ya Kilimo
inatarajia kutoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa wakulima
ambayo itakuwa ni ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu na kwa riba nafuu
(kati ya asilimia 7 hadi 12 kwa mwaka).” Alisema Bw. Semkyi.
Aidha, Bw. Semkyi alifafanua kuwa
mikopo hiyo inalenga kuwanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa
kwa ajili ya kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa
ongezeko la thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya
misitu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa Benki hiyo Bw. Robert Pascal alisema
kuwa kwa miradi mikubwa ya kilimo inayoendeshwa kati ya Serikali,
Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, mikopo ya moja kwa moja itatolewa
kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo hasa kuimarisha mifumo ya
minyororo ya kuongeza thamani katika mazao ya kilimo.
Pia Bw. Pascal alieleza kuwa Benki
hiyo itatumia bidhaa mbalimbali zenye ubunifu katika kuwezesha vikundi
vya wakulima wadogo, wafugaji wa ng’ombe, samaki na kuku.
Benki ya Kilimo Tanzania (TADB)
imeanzishwa mwaka 2014 kwa madhumuni ya kutekeleza Sera za Serikali
kuhusu upatikanaji wa fedha za kuendeleza kilimo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni