Ijumaa, 23 Septemba 2016

JUMAA AUNGANA NA WAKAZI SOGA KUMKATAA MENEJA WA MWEKEZAJI MOHAMMED INTERPRISES


jumaa2
Mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizungumza na wakazi wa kata ya Soga ,kuhusiana na mgogoro wao baina ya meneja wa mwekezaji Mohammed interprises ,Amir Mndeme pamoja na mgogoro wa wakazi hao na mwekezaji uliodumu kwa miaka 21 sasa.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
jumaa4
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama, akizungumza na wakazi wa kata ya Soga ,kuhusiana na mgogoro baina yao na meneja wa mwekezaji Mohammed interprises Amir Mndeme pamoja na mgogoro uliodumu kwa miaka 21 sasa juu ya mwekezaji huyo kuhodhi eneo kubwa na kusababisha wananchi kupungukiwa na eneo la  kujishughulisha na shughuli za kijamii ikiwemo kilimo(Picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Soga
MBUNGE wa Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa ,ameungana na wakazi wa kata ya Soga kumkataa meneja anaesimamia eneo la mwekezaji Mohammed Interprises ,Amir Mndeme, anaedaiwa kutishia amani watu ,kudharau serikali na kujitia mungu mtu.
Aidha wameitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina na kuangalia upya umiliki wa eneo la mwekezaji huyo ambalo lina ukubwa wa hekta 20,000 na kusababisha wananchi kupungukiwa  na maeneo ya kujishughulisha ikiwemo kilimo.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi ,katika kijiji cha Soga,Jumaa alisema mgogoro baina ya wananchi kata ya Soga na Mohammed Interprises umedumu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Alisema mgogoro huo umefikia pabaya kwani vijana 16 wamekamatwa na polisi kwa madai ya kuchimba mchanga kwenye eneo la mwekezaji hali iliyosababisha wananchi kuifunga ofisi ya serikali ya kijiji kwa siku mbili kutokana na kutokuwa na imani nayo.
Jumaa alieleza kufuatia kutokea kwa matukio hayo alilazimika kwenda eneo la tukio ambapo wananchi walisema hawafungui ofisi hiyo hadi viongozi wa wilaya ama mkoa wafike kusikiliza kilio chao.
“Mgogoro huu kwasasa unakua na kuhofia kupoteza amani iliyopo,imefikia hatua ya meneja wa MO kutumia polisi kunyanyasa wananchi na upande wa wananchi kuweka chuki nae”
‘Tangu aletwe meneja mpya bwana Mndeme, amekuwa akitishia amani na kutumia nguvu za pesa kunyanyasa wananchi.Mameneja hapa wameshakuja zaidi ya sita lakini meneja huyu amekuwa kero kubwa”alisema Jumaa.
Mndeme amekuwa akikataza watu kukatisha katika eneo lake,kuchimba mchanga kwenye machimbo ya mchanga ambayo anadai yapo kwenye eneo hilo na kupelea kuwanyima uhuru wananchi.
“Machimbo hayo ni ya asili ,vijana wanajitafutia kipato lakini yeye anakataza watu wasichimbe na kutumia polisi kuwakamata ambapo juzi walikamatwa vijana 16 ”alisema Jumaa.
Jumaa alisema hatua zichukuliwe haraka pamoja na mwajiri Mohammed inteprises amwondoe meneja wake ili kurejesha amani kwa jamii.
Nae mtendaji wa kata ya Soga, Betram Mfalamagoha,alisema septemba 20 baadhi ya polisi walioambatana na Mndeme walienda kuwakamata vijana 16 ,waliokuwa wakichimba mchanga kwenye machimbo ya mchanga.
Alisema kijana mwingine aligongwa na gari la mikopo kisha, askari polisi walikwenda na kuendelea kumpiga kijana huyo licha ya kuwa amegongwa na sasa yupo Tumbi hospital kwa matibabu.
Wakazi wa kata hiyo, akiwemo Hussein Maro,Ramadhani Rashid ,Iddi Muhunzi na mwenyekiti wa kijiji cha Kipangege Shomary Mwinshehe ,walisema wamechoshwa na tabia anazozifanya meneja Mndeme.
Walisema baadhi ya polisi wamewekwa mkononi kwani wamekuwa wakitumika na meneja huyo kwenda kuwakamata wananchi na kuwashurutisha bila kosa.
Mzee Omary Kibwana ,alisema anaimani na serikali kuwa itaangalia suala hilo kwa kina ili kuleta suluhisho la mgogoro huo wa kipindi kirefu.
Mkuu wa kituo cha polisi Kibaha,Emmanuel Bondo ,alisema kazi yao ni kulinda amani kwa watu wote bila kupendelea.
Kamanda Bondo alisema ,kutokana na malalamiko aliyofikishiwa atayafanyia kazi na kuahidi kushirikiana na wananchi hao pale patakapokuwa na tatizo.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alifika katika eneo hilo na kutoa agizo kuwa meneja Mndeme aondoke kuanzia sasa na mwajiri wake atafute meneja mwingine.
Alisema hakuna jeuri zaidi ya serikali na serikali haiwezi kumvumilia mtu mmoja ambae anatishia maisha ya watu na kuwajengea hofu ya kuishi.
Assumpter alieleza hakuna mungu mtu zaidi ya wananchi na sasa yeye ndie atakuwa saizi yake huyo meneja anaetikisa kata nzima kwa pesa zake.
Aliomba wananchi wasibuguziwe na kuwataka polisi wasiwe wepesi wa kuhongwa kitu kidogo kwa ajili ya kuwakandamiza wananchi.
Assumpter alitoa pole kwa kijana aliyegongwa na gari la mikopo  kisha kupigwa tena na polisi kwa madai ya kuingia kwenye eneo la MO, na kuongeza kuwa amesikitishwa na vitendo vya meneja huyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuanzia sasa Mndeme aondoke,na kuwaasa wananchi wasifanye fujo wala maandamano bali watulie na serikali ipo kwa ajili yao.
Mndeme alipatikana kwa njia ya simu na kusema hawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na vitisho ambavyo ameshaanza kuvipata,na baada ya kujibu hayo alikata simu.
Baada ya mkutano huo wananchi waliamua kutoa magogo na makuti waliyofunga kwenye ofisi ya serikali ya kijiji ambayo waliifunga kutokana na sakata hilo.

Masauni apanda mabasi ya Mwendo Kasi jijini Dar es Salaam


drt1
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akikata tiketi ya mabasi ya Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya UDA-RT katika Kituo cha Ubungo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri na mabasi hayo kutoka katika kituo hicho kuelekea Posta. Kushoto ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga naye akiwa mmoja wa wasafiri wa mabasi hayo. Masauni aliyapanda basi la Mwendo kasi mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
drt2
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiigusisha tiketi yake katika mashine ya Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya UDA-RT katika Kituo cha Ubungo jijini Dar es Salaam ili mruhusu kuingia ndani ya stendi hiyo kwa ajili ya kusafiri na mabasi hayo kutoka katika kituo hicho kuelekea Posta. Mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
drt3
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiingia ndani ya Basi la Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya UDA-RT katika Kituo cha Ubungo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri na basi hilo kuelekea katikati ya Jiji, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
drt4
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni  akiwa ndani ya moja ya mabasi ya mradi wa mabasi ya mwendo kasi ya UDA-RT jijini Dar es Salaam akitoka kituo cha Ubungo kuelekea katikati ya Jiji, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
drt5
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni  akitelemka katika moja ya mabasi ya mradi wa mabasi ya mwendo kasi ya UDA-RT jijini Dar es Salaam katika kituo cha Nyerere, Posta. Masauni alipanda basi hilo akitokea Ubungo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
drt6
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni  akiondoka katika Kituo cha Mabasi ya Mwendokasi cha Nyerere, Posta, mara baada ya kusafiri na usafiri huo akitokea Ubungo, jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria. Katikati ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………………….
Felix Mwagara, MOHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameupongeza Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya UDA-RT wa jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi waendelee kuyatumia mabasi hayo wanaposafiri sehemu mbalimbali jijini humo.
Mhandisi Masauni ameyasema hayo jana mara baada ya kusafiri na mabasi hayo kutoka kituo cha mabasi hayo cha Ubungo mpaka katikati ya jiji kwa lengo la kujionea jinsi mabasi hayo ya mwendokasi yanavyohudumia abiria pamoja na kuwapa moyo wananchi kuwa usafiri huo unatumiwa na mwananchi wa aina yeyote.
Akizungumzia usafiri huo, Masauni alisema mradi huo umerahisisha sana usafiri kwani ametumia dakika chake akitokea Ubungo hadi Posta katikati ya jiji bila usumbufu wowote, hivyo mradi huo ameomba uendelee kulindwa pamoja na kutunzwa na UDA-RT na wananchi wenyewe kwa ujumla.
“Mimi kwa kweli nimeufurahia sana usafiri huu, Serikali imefanya jambo kubwa sana kwa wananchi wake, kwa kuwajali wananchi kwa kuuleta mradi huu ambao unarahisisha safari kwa uharaka zaidi na pia unapendezesha jiji kwa jinsi magari yalivyo nadhifu,” alisema Masauni ambaye pia alilipa nauli kwa kupanga foleni kama wananchi wengine wanavyofanya wanapotaka kusafiri na usafiri huo.
Masauni aliongeza kuwa; “Nimefarijika sana na lugha ya adabu na tulivu ambayo wanaitumia madereva wa mabasi hayo wanapowatangazia wananchi vituo mbalimbali vya kushuka na kuingia kwenye mabasi hayo, hii inasaidia kuwa na mawasiliano mazuri na abiria, pia inaonesha madereva hao wamefunzwa vizuri na wanaipenda kazi yao.”
Hata hivyo, Masauni alitoa ushauri kwa uongozi wa mabasi hayo, kuruhusu wananchi waingie ndani ya mabasi hayo kwa idadi ambayo haitaleta kero kwa abiria wengine ili kupunguza wingi wa abiria hao kwa lengo la kuepuka mbanano mkubwa wa abiria.
Pia aliwataka wananchi wa jiji hilo kuyatunza mabasi hayo, na pia kukubali maelekezo ya madereva wanapotoa matangazo wanapokuwa safarini kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji.
Naibu Waziri huyo alipanda mabasi hayo akitokea Ubungo mara baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza kwa kutembelea Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kwa lengo la kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria wanaosafiri na mabasi hayo.  Masauni pia alifanya ziara hiyo ya ghafla kwa kutembelea Stendi ya Kibaha, mkoani Pwani.

JUMA NATURE, PETER MSECHU KUTUMBUIZA TAMASHA LA SIKU YA MSANII WA TANZANIA KIJIJI CHA MAKUMBUSHO


index 
Msanii Juma Nature ambaye ni mmoja wa wasanii watakaotumbuiza katika Siku ya Msanii wa Tanzania kesho Septemba 24 kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam.
……………………………………………………………………..
Na Herieth Semgaza
Katika  kuadhimisha siku ya msanii wa Tanzania , kwa mara ya kwanza hapa nchini Tamasha la sikuMsanii wa Tanzania litafanyika Septemba 24 katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, Siku hii itawakutanisha wasanii wa sanaa aina mbalimbali katika jukwaa moja .
Augustino Makama ambaye ni mratibu wa Tamasha la Siku ya Msanii wa Tanzania kutoka BASATA  ametoa ufafanuzi wa mambo kadhaa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es salaam
 Augustino Makama afisa sanaa BASATA  amesema kuwa siku ya msanii inawakutanisha wasanii wa sanaa ya Mziki, Filamu, Ufundi, na Maonyesho.ilikuonyesha umahiri na uwezo wao kwa hadhira wawapo katika jukwaa.
Aidha ameongeza Kuwa mradi huu umebuniwa na Balaza la Sanaa la Taifa  BASATA lengo lake kubwa likiwa ni kutambua, kuhamasisha na kuthamini kazi zinazotolewana na wasanii wa Tanzania.
Kauli mbiu ya “Nguvu ya Sanaa”Itakayo jumuisha mtiririko wa matukio ambapo tayari maadhimisho hayo yalishazinduliwa tangu tarehe 26 Mei 2016 na Waziri wa Habari, Sanaa ,Utamaduni na Michezo Mh Nape Nauye.kwa uwakilishi wa katibu wa wizara hiyo Profesa Elisante Ole Gabriel . 
                      Maadimisho yatafanyika katika kijiji cha Makumbusho ya Taifa Kijitonyama jijini Dar es salaam yakidhaminiwa na kampuni ya  HAAK NEEL PRODUCTION LTD                         
 Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa  tarehe 29 Ocktoba 2016 ambapo wasanii mbalimbali watapewa tuzo kutokana navigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kupata wasanii wenye kazi bora na zenye viwango.
Tamasha hilo  litaburudishwa na wasanii Juma Nature, Peter Msechu, Misoji pamoja na wasaniii wengine watakao kuwepo jukwaani ili kuwapa burudani waalikwa watakaohudhuria , Katika Tamasha hilo hakutakuwa na  kiingilio ambapo litaanza saa tatu asubuhi mpaka saa tatu usiku

MALI ZILIZOPATIKANA KWA NJIA YA RUSHWA NA UFISADI KUTAIFISHWA


mun
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akiongea na vyombo vya habari kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania hivi karibuni. (Picha ya Maktaba).
……………………………………………………………………………………………
Makala iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) aliongea kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini, pamoja, Matumizi ya Nyaraka za Serikali na Maadili kwa viongozi kwa viongozi wa Umma. Waziri Kairuki aliongea hayo katika Runinga ya Taifa (TBC), makala ya leo ni sehemu ya mwisho na inaangalia mapambano dhidi ya rushwa na mpango wa kunusuru kaya masikini hapa nchini.
Mapambano dhidi ya rushwa
Waziri Kairuki alieleza Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini mfano kwa kufuatilia fedha za Miradi ya Maendeleo kupitia Ofisi za Kanda za TAKUKURU kwa lengo la kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inaendana na kiasi cha fedha kilichotolewa ambapo ufuatiliaji huo umeiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 39.34.
“Tumewasilisha majalada 297 kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ajili ya kuombewa kibali cha mashitaka ambapo majalada 229 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani” Waziri Kairuki alifafanua.
Aliongeza mikakati ya serikali ni pamoja na kuhuisha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Na. 11 ya 2007 ili kujumuisha makosa ya uhujumu uchumi na kutaifisha mali zilizopatika na kwa njia ya Rushwa na Ufisadi.
Kuhusu kaya masikini hali ikoje?
Waziri Kairuki alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ambao utachukua miaka kumi unatekelezwa katika Halmashauri zote za Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.
“Katika kipindi cha miaka minne mpango umetekelezwa Vijiji, Mitaa na Shehia 9,960 ambayo ni sawa na wastani wa asilimia 70. Kaya 1,358,268 zimetambuliwa ambapo kati ya hizo, Kaya 1,110,377 zimeandikishwa” Waziri Kairuki alisena na kuongeza kaya 1,110,377 zimehawilishiwa fedha kwa kulipwa ruzuku katika awamu 16 ili kuziwezesha kuwekeza katika lishe, afya na elimu.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi unatekelezeka?
Waziri Kairuki alisema Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership) ulianza kutekelezwa nchini toka mwaka 2012/13, na umejikita katika kuweka uwazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali; Ushirikishwaji wa Sekta za Umma na Binafsi katika utekelezaji wa Mpango; Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi; Matumizi ya Teknolojia na Ubunifu; na Mapambano dhidi ya Rushwa.
Alisema miongoni mwa yaliyofanyika ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi kuhusu bajeti ya Serikali kwa kuandaa kijitabu cha  “Citizen budget” kilichoandaliwa kwa Kiswahili na  lugha rahisi kwa kuchapishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Pia, taarifa za utekelezaji za sekta za kipaumbele Afya, Elimu na Maji kuchapishwa katika Tovuti za sekta hizo na kukamilika kwa zoezi la upembuzi yakinifu wa Takwimu Huria (Open Data) ili  kuongeza uwazi wa takwimu na taarifa mbalimbali;
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi kwa mikakati mbalimbali ikiwamo, kuendelea na utekelezaji wa kuwa na uwazi katika bajeti ya Serikali kwa kuweka taarifa za bajeti kwenye tovuti mbalimbali kwa lugha nyepesi na kwa Kiswahili na kuimarisha mfumo wa Takwimu Huria ambayo utarahisha wadau mbalimbali kupata takwimu zinazohusu masuala mbalimbali hususan Afya, na Elimu.
Majukumu ya Ofisi ni yapi?
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) ina majukumu ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma; Taratibu, Miundo na Mifumo ya Utoaji Huduma; Uendelezaji Rasilimaliwatu; Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka katika Utumishi wa Umma. Aidha, Ofisi hii inasimamia maadili ya Watumishi na viongozi wa Umma; mapambano dhidi ya  rushwa; Mfuko wa Maendeleo ya Jamii; Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge; Mfuko wa Rais wa Kujitegemea; na Taasisi ya Uongozi.

Alhamisi, 22 Septemba 2016

TUNDURU YAKABIDHIWA OFISI YA MADINI




Na Zuena Msuya, Tunduru ,RUVUMA, 


Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini(SMMRP) imepokea jengo la ofisi ya Madini Mkazi wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kutoka kwa kampuni ya ukandarasi ya Mkongo Contractors ili kuanza kutumika na ofisi hiyo baada ya kufanyiwa ukarabati .

Akizungumza mara baada ya kupokea jengo hilo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma hivi karibuni, Msanifu Majengo wa SMMRP , Joseph Ringo alisema kuwa lengo la kufanya ukarabati katika jengo hilo ni kuimarisha shughuli za kiutendaji katika uendelezaji wa shughuli za madini wilayani ya Tunduru na viunga vyake ukizingatia kuwa wilaya hiyo imejikita zaidi katika uchimbaji wa madini ya vito vya aina mbalimbali.

Aidha Msanifu majengo Ringo Alifafanua kuwa kama ilivyo dhamira ya mradi wa SMMRP ,kufanyika kwa ukarabati katika jengo hilo kutawezesha Afisa Madini Mkazi wa eneo hilo kufanya kazi zake kwa ufanisi na kufikia malengo aliojiwekea katika kuwahudumia wadau wa madini.

Vilevile alisema kuwa ukarabati wa jengo hilo umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ambao umejumuisha vifaa vya kisasa ikiwemo kuunganishwa na mfumo mpya na wa kisasa wa TEHAMA ambao unarahisisha utunzani wa kumbukumbu za wadau wa madini tofauti na ilivyokuwa hapo awali. 

Kwa upande wake Ofisa Madini mkazi Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi aliupongeza mradi wa SMMRP kwa kuboresha na kuzijengea uwezo ofisi za madini nchini ili kuboresha shughuli za uendelezaji wa rasilimali za madini.

Hata hivyo Mhandisi Mwanjisi ameushauri mradi wa SMMRP,kutumia muda mfupi katika kutekeleza shughuli zake za ukarabati na ujenzi wa majengo mbalimbali kwa lengo la kuendeleza rasilimali madini.

Naye Mkurugenzi Msaidizi rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini,Joyceline Lugora, amewataka maafisa madini wakazi na wakanda zote nchini kutunza miundombinu ya majengo hayo ili kuondoa gharama za ukarabati wa mara kwa mara.

Na pia ichukue muda mfupi kukarabati eneo lililoharibika endapo kumetokea uharibufu katika jengo



Taswira tofauti za muonekano wa jengo la Ofisi ya Madini Mkazi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, jengo hilo limejengwa na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini ( SMMRP) unaotekelezwa na Benki ya Dunia.



Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini,Wasanifu majengo pamoja na Wakandarasi waliojenga jengo la ofisi ya madini Mkazi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakifanya ukaguzi wa jengo hilo kabla ya kukabidhiana ili lianze kutumiwa na Ofisi ya Madini Tunduru, jengo hilo litazinduliwa rasmi hivi karibuni.
Wawakilishi wa kampuni ya wakandarasi, wasanifu majengo pamoja na washauri waliotekeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Madini Mkazi wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakijirisha kusoma ramani kabla ya kukabidhi jengo hilo kwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia mradi wake wa SMMRP. 
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini,Wasanifu majengo pamoja na Wakandarasi waliojenga jengo la ofisi ya madini Mkazi wilani Tunduru mkoani Ruvuma wakifanya ukaguzi wa jengo hilo kabla ya kukabidhiana ili lianze kutumiwa na Ofisi ya Madini Tunduru, jengo hilo litazinduliwa rasmi hivi karibuni.
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini,Wasanifu majengo pamoja na Wakandarasi waliojenga jengo la ofisi ya madini Mkazi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakifanya ukaguzi wa jengo hilo kabla ya kukabidhiana ili lianze kutumiwa na Ofisi ya Madini Tunduru, jengo hilo litazinduliwa rasmi hivi karibuni.

Msanifu Majengo wa SMMRP , Joseph Ringo akitia saini hati za makabidhiano ya jengo la ofisi ya Madini Mkazi Wilani Tunduru mkoani Ruvuma,( kulia) akishuhudiwa na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Mhandisi Fred Mahobe( wa pili kulia).
Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini Joyceline Lugora ( mstari wa mbele wa pili kushoto) akikabidhi ufunguo wa jengo la ofisi ya Madini Mkazi Wilani Tunduru mkoani Ruvuma, kwa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Mhandisi Fred Mahobe,( mstari wa mbele wa pili kulia) mara baada ya kukabidhiwa kutoka  kiongozi wa timu ya ushauri ya ujenzi wa jengo hilo, Msanifu Majengo Paul Mshana (kushoto katikati) aliyepewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa jengo hilo. 

Tanzania yaahidi mazingira mazuri ya uwekezaji Sekta ya Madini



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida (Wa pili kutoka kulia), Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje (Wa kwanza kushoto), Watendaji kutoka Serikali ya Japan na JOGMEC wakati wa semina iliyolenga katika uendelezaji endelevu wa rasilimali madini nchini.
Meneja wa Kanzidata na Uchakataji wa Taarifa za Jiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia (GST), Terence Ngole akizungumza wakati wa Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida (wa kwanza kulia) akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani) akifungua Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Wadau mbalimbali waliohudhuria Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Wadau mbalimbali waliohudhuria Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe akifungua Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.


Teresia Mhagama na Devotha Myombe

Tanzania imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kama ilivyoainishwa katika Sera ya Madini ya mwaka 2009.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe wakati wa semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji endelevu wa rasilimali madini nchini.

Alisema kuwa, Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 imelenga katika kuanzisha migodi mikubwa, ya kati na midogo inayoendeshwa kwa kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira hivyo mazingira mazuri ya uwekezaji yatavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza ili kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

Profesa Mdoe alisema kuwa semina hiyo ililenga katika kupata taarifa zilizohuishwa kutoka Japan na Tanzania kuhusu shughuli za utafiti na utunzaji wa mazingira katika Sekta ya Madini nchini na kujadiliana juu ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi husika.

“Semina hii ni muhimu kwani Taasisi hizi zitajadiliana kuhusu kuendeleza ushirikiano katika sekta hii, kufahamu fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Madini kwani wadau kutoka Tanzania na Japan wataweza kupata taarifa za utafiti kuhusu madini yaliyopo nchini na pia Taasisi ya JOGMEC itapata fursa ya kueleza shughuli zake barani Afrika,” alisema Profesa Mdoe.

Akieleza kuhusu Sekta ya Madini nchini, Profesa Mdoe alisema kuwa Sekta hiyo kwa sasa inachangia asilimia 3.5 katika Pato la Taifa na kueleza kuwa asilimia hiyo bado ni ndogo kwani lengo la Serikali ni kuona kuwa Sekta hiyo inachangia mpaka asilimia 10 kufikia mwaka 2025.

Hata hivyo Profesa Mdoe alisema kuwa ili sekta hiyo ichangie ipasavyo katika Uchumi wa Taifa, kutategemea kutoshuka kwa bei ya bidhaa zinazotokana rasilimali madini na uchumi wa dunia kuendelea kukua ili makampuni yanayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa madini yapate fedha kutoka Taasisi za kifedha duniani ili kuanzisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini.

Aidha Profesa Mdoe aliwaalika wawekezaji kujenga vituo vitakavyotumika katika shughuli za uongezaji thamani madini ya Tanzania kwani alisema kuwa uongezaji thamani madini ndani ya nchi utasaidia kuongeza ajira kwa wananchi, ubadilishanaji wa teknolojia kutoka nchi zilizobobea katika shughuli hizo na kuwezesha ukusanyaji wa kodi ambayo itasaidia katika shughuli nyingine za maendeleo.

Awali Meneja wa Kanzidata na Uchakataji wa Taarifa za Jiolojia kutoka GST, Terence Ngole, alieleza JOGMEC na GST walisaini Mkataba wa Makubaliano mwaka 2010 ambapo mashirikiano kati ya Taasisi hizo yamesaidia kuongeza utaalam na teknolojia katika utafiti wa madini kupitia mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na mfupi yanayotolewa na Shirika la JOGMEC.

Alisema kuwa Semina hiyo imeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Japan na Tanzania ambao wanajishughulisha na Sekta ya Madini na Mazingira na kwamba ni semina ya kwanza kuendeshwa nchini na Shirika la JOGMEC.

IGP MANGU AFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI GEITA

 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akiwa ameambatana pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Geita, jana wakati alipotembea ofisi za Mkuu wa mkoa wa Geita, Meja Jenerali (Mst) Ezekiel E. Kyunga (watatu kutoka kushoto),  IGP Mangu yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi.
  Mkuu wa mkoa wa Geita, Meja Jenerali (Mst) Ezekiel E. Kyunga, akitoa neno la ukaribisho kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, ambaye yupo katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi, anayefuata ni kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, SACP Mponjoli Mwabulambo.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akifuatilia jambo kwa makini kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Geita, Meja Jenerali (Mst) Ezekiel E. Kyunga, pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo jana akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akitoa neno mbele ya kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Geita, jana wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akiweka sahihi katika kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita, kwa ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu  ya kipolisi mkoani humo, katikati ni Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhe. Shaaban Ntarambe, akifuatiwa na kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, SACP Mponjoli Mwabulambo.
  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, pamoja na timu ya maofisa na kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, SACP Mponjoli Mwabulambo, wakimsikiliza kwa umakini Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhe. Shaaban Ntarambe, alipomtembelea ofisini kwake jana wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akiwa katika kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Chato mkoani Geita, jana alipotembelea kituo hicho wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kipolisi. (Picha zote na Demetrius Njimbwi - Jeshi la Polisi)