Jumatano, 7 Oktoba 2015

TANESCO:MGAWO WA UMEME MWISHO OKTOBA 20.


Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Felchesmi Mramba akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ambapo alieleza  juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika kutatua kero ya umeme nchini.


 



SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendeleza juhudi ya kuboresha  upatikanaji wa umeme nchini kwa kuzalisha megawati 35 katika gridi ya Taifa jana mchana.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Felchesmi Mramba ameeleza kuwa juhudi za kuhakikisha upatikanji wa umeme unakuwa wa uhakika zinaendelea ambapo megawati 90 zinatarajiwa kuzalishwa wiki hii.

 “Katika kuhakikisha hali ya umeme inarejea kama zamani tunatarajia kuzalisha megawati 70 kupitia mitambo ya Kinyerezi na megawati 20 kupitia mitambo ya Symbion na hivyo kufanya jumla ya megawati 90 hii itapunguza ugumu wa upatikanji wa umeme nchini” alisema Mramba.

Aidha aliongeza kuwa kufikia tarehe 20 Oktoba mwaka huu uzalishaji wa umeme nchini  utakuwa wa kutosha  kutokana na jitihada  mbalimbali zinazofanywa na Tanesco .

Vilevile alieleza kuwa upungufu wa umeme unatokana  na kupungua kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme kwa asilimia 81.3 na hivyo kupelekea tatizo la kukati kwa umeme mara kwa mara.

 Mramba  ametoa wito kwa wananchi na wateja wa Tanesco  kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki cha upungufu wa umeme kwa kuwa juhudi madhubuti zinaendelewa kufanywa kuhakikisha hali hii inatatuliwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni