WAZIRI MKUU AONGOZA WAKAZI WA DODOMA MAZISHI YA ASKOFU ISUJA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitoa heshima za mwisho kwa Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma,
Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la
Mtakatifu Paul wa Msalaba Aprili 20, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri
Muu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo la Dodoma , Beatus Kinyaiya katika
mazishi ya Askofu Mstaafu wa Dodoma Mathias Isuja yaliyofanyika kwenye
kanisa kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Mjini Dodoma Aprili 20, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la
Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu
la Mtakatifu Paul wa Msalaba, Aprili 20, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameongoza maelfu ya waumini na wakazi wa mkoa wa Dodoma katika mazishi
ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu
la Dodoma.
Amesema kifo hicho ni pigo kwa watu wote na si kwa kanisa pekee kwa sababu walimtegemea kulisaidia Taifa kiroho na kimaendeleo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatano, Aprili 20, 2016) wakati akizungumza na waumini na wakazi wa
mkoa huo na mikoa jirani kwenye ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye
Kanisa la Kiaskofu la Mtume Paulo wa Msalaba mjini Dodoma.
Askofu Isuja ambaye alizaliwa
Agosti 14, 1929 alikuwa Askofu wa kwanza mzalendo katika Jimbo la Kanisa
Katoliki la Dodoma. Alistaafu kazi ya uaskofu mwaka 2004 kwa mujibu wa
sheria ya kanisa. Alifariki Aprili 13, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa
uhai wake na kuyaendeleza yote aliyoyaanzisha kwenye maeneo aliyowahi
kuyatumikia.
“Tumepoteza mtu makini, sisi ni
mashahidi wa mchango mkubwa wa marehemu siyo tu katika kutoa huduma za
kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga kuleta maendeleo kwa
wananchi katika jimbo hili la Dodoma na katika taifa kwa ujumla,”
amesema.
Mapema, akitoa mahubiri wakati wa
ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Judathadeus
Ruwa’ichi alisema waumini wa kanisa hilo wa mkoa wa Dodoma na Tanzania
nzima wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomjalia
Askofu Isuja.
“Tunapaswa kumshukuru kwa maisha
marefu ambayo Mungu alimzawadia baba yetu Isuja. Katika Zaburi ya 90
tunasoma kuwa mwanadamu ana miaka ya matazamio ambayo ni 70, lakini yeye
alipewa miaka ya matazamio 70 na akazawadiwa nyongeza ya miaka 10 na
kisha miaka mingine sita na nusu,” alisema.
Alisema zawadi nyigine ambayo
Mungu aliwapatia waumini hao ni ya imani ambayo Baba Askofu Isuja
aliipokea, aliifundisha na aliishi na akawataka waendelee kumshukuru
Mungu kwa hilo. “Miaka 56 ya utumishi wake kama padre na askofu ni
zawadi kwa Dodoma na Tanzania na siyo kwake yeye binafsi,” alisema.
Ibada hiyo ya mazishi
ilihudhuriwa na Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa kawaida 28 kutoka majimbo
ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Mpanda, Iringa, Songea, Tabora,
Morogoro na Mahenge. Mengine ni Musoma, Rulenge, Mbinga, Moshi, Same,
Kahama, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara na Lindi. Majimbo mengine ni
Bukoba, Tanga, Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Kondoa na
Kayanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni