Uchukuzi SC yang’ara Mei Mosi
Kikosi cha Uchukuzi SC kabla ya mechi na Ukaguzi.
Benchi la timu ya Uchukuzi SC wakiwa wanafuatilia mchezo dhidi yao na Ukaguzi..

2808: Wachezaji wa timu
mbalimbali za Uchukuzi SC wakishangia mara baada ya mchezo wa soka dhidi
ya Ukaguzi kumalizika. Uchukuzi iliibuka mshindi kwa magoli 3-1


…………………………………………………………………………………………
TIMU ya soka ya Uchukuzi SC
imeng’ara kwa kuifunga Ukaguzi mabao 3-1 katika mashindano ya Mei Mosi
yanayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Uchukuzi SC ambayo chini ya
benchi la ufundi mahiri linaloongozwa na Kenneth Mwaisabula ‘Mzazi’
ambaye ni Mkuu wa benchi hilo, huku Elutery Muholeli ni kocha na Robert
Damian ni meneja wa timu hiyo, waliwapeleka puta wapinzani wao na
kuandika bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Kado Nyoni, baada ya
kuwahi mpira wa kona safi iliyochongwa na Omar Said ‘Chidi’ katika
dakika ya 34.
Hatahivyo, Ukaguzi walisawazisha
katika dakika ya 50 kupitia kwa Ben Chezue aliyepiga mpira wa adhabu
ndogo uliokwenda moja kwa moja golini. Chezue aliingia dakika 49
kuchukua nafasi ya Deo Masanja aliyekuwa ameumia.
Uchukuzi SC iliongeza bao katika
dakika ya 72 lililofungwa Issac Ibrahim aliyeachia shuti kali,
lililomshinda kipa wa Ukaguzi, Shomari Dumba.
Nahodha wa Uchukuzi SC, Francis
Charles alipigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la tatu katika
dakika ya 90 kwa njia ya penati baada ya Bilal Mleli kushika mpira
katika eneo la hatari.
Uchukuzi SC iliyokuwa ikicheza
kwa kuonana, awali timu Uchukuzi SC ilikosa magoli kibao ya wazi, baada
ya wachezaji wake Abubakar Mwamonchi katika dakika ya 25 kupiga mpira
uliopita pembeni kidogo ya goli, huku Francis alishindwa kuunganisha
krosi ya Masoud Juma katika dakika ya 30, tena Francis aliyeisumbua
ngome ya Ukaguzi katika dakika ya 58 alipaisha mpira akiwa karibu na
kipa.
Akizungumza mara baada ya mechi,
kocha Muholeli alisema Ukaguzi ni moja ya timu ngumu, lakini
aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutoka na ushindi
mnono, ambao umesaidia kusafisha njia.
“Hapa tumekuja kushindana na kila
mechi kwetu tunaiita ni fainali, hivyo timu zote zilizokuja hapa ni
nzuri, ila tunataka tushinde mechi zote ili tujiweke pazuri kushinda na
kutwaa kombe hili, kwani tumeshafika fainali mara nne,” alisema
Muholeli.
Naye Mwenyekiti wa Uchukuzi SC,
Mohamed Ally alisema wamekuja Dodoma kuchukua ubingwa na anauhakika wa
timu yake itafanya vyema kutokana na nidhamu ya mazoezi wanayofanya kila
siku.
Kikosi cha ushindi cha Uchukuzi
SC ni: Barton Willy, Ally Poloto, Omar Said ‘Chidi’, Godwin Ponda, Kado
Nyoni, Fidelis Kyangu, Seleman Kaitaba/Issac Ibrahim (63), Francis
Charles, Ramadhani Madebe, Abubakar Mwamachi/Omar Kitambo (35), na
Masoud Juma/Michael Bernad (46).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni