Jumatano, 20 Aprili 2016

Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar imeanza kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar kuwalipa wazee posho

zan
Na Masanja Mabula –Pemba 
SERIKALI  ya Mapnduzi ya Zanzibar imeanza kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein la kuwalipa posho la shilingi 20,000/- wazee wote wenye umri kuanzia miaka 70 .
Katika Wilaya ya Wete zoezi hilo limefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jamhuri ambapo zaidi ya wazee 200 , kutoka shehia ya Sellemu ,  Kipangani , Limbani , Mtemani , Bopwe na Utaani  walijitokeza kwa ajili ya kulipwa posho hizo .
Wakizungumza na mwananchi jana nje ya Ukumbi huo kwa nyakati tofauti  , baadhi ya wazee wamemshukuru Rais wa Zanzibar  kwa kutimiza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni zilizofanyika mwaka jana .
Wamesema kuwa Serikali imetimiza wajibu wake kwa wananchi , na kuongeza kwamba posho hilo litawasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili katika familia zao .
Khamis Rajabu Msellem (73)  alisema kwamba  pamoja na changamoto zilizopo lakini Rais Shein  anapaswa kuangalia zaidi mwelekeo wa Serikali yake pamoja na maendeleo ya wananchi anaowaongoza  .
“Kwa hili Serikali imetimiza wajibu wake wa kutukumbuka sisi wazee , kiwango cha shilingi 20,000/= kinatosha sana kumtatulia mzee baadhi ya changamoto , kwa mpango huu sina budi kumpongeza Rais wetu ”alisema Mzee Khamis mkaazi wa Bopwe.
Naye Time Khalfan Khamis (72) amesifu mpango kwani hauna chembe ya ubaguzi na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za rais shein kwani zimelenga katika kuwakomboa wazee kwani baadhi yao  wamekosa  msaada kutoka kwa familia zao.
Alisema miaka ya nyuma kila mzee alikuwa akipewa posho la shilingi mia tano (500) kwa mwezi kiwango ambacho kilikuwa hakimsaidii Mzee katika kutatua changamoto za maisha .
“Awali tulikuwa tunapewa shilingi 500/= kwa mwezi hela ambayo ilikuwa inatumika kununulia tumbaku na kumalizika , lakini hii leo tunapewa 20,000/= alhamdulilah tunamshukuru Rais wetu ”alieleza Time mkaazi wa Mtemani .
Aidha Mzee Mcha Omar Bweni (74)  alisema wazee waliowanyonge wamepata nafuu wa maisha , na kuongeza kwamba licha ya fedha hizo kuwa haiwezi kabisa kumaliza  shida na matatizo yanayowakabili .
Naibu wa Sheha wa Shehia ya Sellem Shaban Mpangile aliliambia mwananchi kwamba zoezi hilo linaenda kwa amani na utulivu na kila mzee aliyeandikishwa baada ya kutimiza masharti atanufaika na mpango huo .
Alisema zoezi la ulipaji wa posho kwa wazee wenye umri kuanzia miaka 70 , linakwenda kwa mpangilio na utaratibu maalumu ambapo baadhi ya shehia watalipwa kesho (leo) na hii imepangwa ili kupunguza masongamano.
“Zoezi hili limegawanywa kwa zone , ambapo baadhi ya shehia zitakuja kesho (leo) na hii imepangwa makusudi ili kupunguza masongamano ”alifahamisha Mpangile .
Utaratibu huu utawafanya wazee kupokea kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili kwa mbili (1,200,000/=) kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Dr Ali Mohammed Shein .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni