Jumatatu, 1 Agosti 2016

WAZIRI MKUU AITAKA WIZARA KUWEKA MIKAKATI YA KUENDELEZA UVUVI KATIKA KINA KIREFU CHA BAHARI

MAJI1WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha wananchi kuvua katika maji ya kina kirefu cha bahari kwa kutumia meli kubwa na za kisasa ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imekuwa ikichukuliwa na wavuvi wenye vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.
Aidha, amezitaka halmashauri zote nchini ziweke mikakati na mipango ya kuifanya mito na maziwa mbalimbali nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli za wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema bado nchi haijaweza kutumia rasilimali hiyo kikamilifu.
Amesema halmashauri zinatakiwa zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha miradi ya kufuga samaki katika maeneo yao na wewezeshwe kupata teknolojia ya ufugaji huo.
Akizungumzia vikundi vya wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa alishauri waelimishwe kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana bora za kisasa za uvuvi ili shughuli zao ziwe na tija.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema wakulima wanatakiwa  kuzingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa na wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.
Akizungumzia kuhusu suala la usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali alipata fursa ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.
Amesema amefurahi kuona wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo wana ari kubwa ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza uchumi wa viwanda.
“Naamini kuwa pamoja na lengo la kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi wataongeza ari ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,” alisema.
Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kushirikisha taasisi za umma na binafsi, mashirika na vikundi vya ujasiriamali katika maeneo yao.
Akizungumzia namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.
Awali Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda na maeneo ya vipando vya mazao mbali mbali yaliyoko katika viwanja hivyo ambapo alisema ameridhishwa na juhudi zilizofanyika katika maandalizi ya maonesho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa uwanja huo.
“Napenda kutoa pongezi za dhati kwa kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za kufanyia maonesho. Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu, Mashirika yetu ya Umma na binafsi; na watu binafsi ambao wamejenga na wanaendelea kujenga majengo mazuri na ya kudumu,” alisema.
Pia alizindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na kusema kuwa uboreshaji wa viwanja hivyo unaonesha jinsi wadau wote katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika wanavyotambua umuhimu wa maonesho hayo kama njia ya kuongeza maarifa na kumuenzi mkulima, mfugaji na mvuvi kwa kutambua mchango wao katika uchumi wa Taifa.
Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo: vijana shiriki kikamilifu   (“HAPA KAZI TU”)        

JPM amaliza mgogoro wa makazi Magomeni Kota

indexNa Jonas Kamaleki, MAELEZO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemaliza mgogoro wa makazi wa Magomeni Kota uliodumu kwa kipindi kirefu.
Hayo yamesbainishwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati akiongea na Kamati ya Mgogoro wa Makazi ya Magomeni Kota mbele ya waandishi wa habari.
“Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefuta hati na mikataba yote inayohusiana na ardhi ya yaliyokuwa makazi ya Magomeni Kota, Dar es Salaam”,alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi Rais ameondoa umiliki wa eneo hilo toka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kumilikisha Serikali Kuu ambayo ndiyo itakayosimamia ujenzi wa nyumba 644 ambazo zitauzwa kwa bei nafuu kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota.
“Tutajenga nyumba 644 na kuwauzia kwa bei ya jengo na siyo ya ardhi ili kuwapeni unafuu katika kununua,”alisema Lukuvi huku akishangiliwa na baadhi ya wakazi wa Magomeni.
Aidha, Lukuvi amesema kuwa anampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kumaliza mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa ameagiza  timu ya wataalamu wa Wizara kupima na kuchora michoro kwa ajili ya ujenzi.
Lukuvi amesema katika eneo hilo zitajengwa nyumba za heshima ambazo kila moja itakuwa na vyumba vitatu ili kukidhi mahitaji ya kifamilia kwani watu hawa wamekaa kwa miaka takribani 50 hadi wameshapata wajukuu. Ameongeza kuwa kila mmiliki wa nyumba hiyo atapewa hati yake hata kama nyumba hiyo itakuwa kwenye ghorofa.
Lukuvi amesema kuwa Rais ameagiza maeneo kama ya Magomeni Kota katika mikoa ishirini ya Tanzania Bara nayo yatakuwa katika mfumo huo wa Magomeni. Kwa mujibu wa Lukuvi wazee ambao wanakaa kwenye nyumba kama hizo sehemu nyingine wasiondolewe kwani hao walikuwa watumishi wa umma hivyo Rais amesema wasibughudhiwe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mgogoro wa Makazi Magomeni Kota, George Abel ameshukur Mhe Rais Magufuli na Wazir Lukuvi kwa kutatua mgogoro huo ambao anadai umewasumbua sana.
Ameahidi kutoa ushirikiana kwa Serikali pindi suala la ujenzi litakapokuwa linaendelea ili kuhakikishaujenzi unaenda haraka.
Naye Wakili ambaye alikuwa akiendesha kesi hiyo kabla ya Mhe. Rais kuingilia kati, Mhe. Twaha Tasilima ameonyesha kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli.
“Rais Dkt Magufuli na Mhe. Waziri Lukuvi ni watu wa vitendo na si maneno na kweli wanawajali wanyonge, nawashukuru sana,”alisema Tasilima.
Uamuzi wa kurudisha eneo hilo kwenye Serikali Kuu umetolewa na Rais Magufuli tarehe 10/7/ 2016.

MAJALIWA AFUNGUA MAONYESHO YA NANENANE MOROROGORO

By Newsroom on August 1, 2016 
NAN1Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akisikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva wakati alipotembelea Banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Monyesho ya Wakulima Nane  mjini Morogoro Agosti 1, 2016,    Kushoto ni mkewe Mary. ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN2Waziri Mkuu, Kassim Majliwa na Mkewe Mary (kulia kwake)wakitazama kilimo cha mbogamboga kwa mtindo wa kilimo kichuguu  wakati walipotembelea banda la Chuo Kikuucha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwenye maonyeshoya Nanenane mjini Morogoro Agosti 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN3Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama viatu vilivyotengenezwa katika gereza la Karanga  mkoani Kilimanjaro wakati alipotembelea  banda la Magereza katika  maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoroo Agosti 1, 2016, kulia ni  Mratibu wa Magereza wa maonyesho hayo na Mkuu wa Gereza la  Mtego wa Simba, Oman Msekwa. (Picha  na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN4Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na mkewe Mary (Kulia kwake) wakatazama bwawa la samaki  na banda la kufugia  bata  wakati alipotembelea banda la Magereza katika monyesho ya  wakulima Nanenane mjini Morogoro Agosti 1, 2016. (Picha na Ofisi ya waziri Mkuu)
NAN5Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa na Mkewe Mary wakitazama mboga zilizokaushwa na mtambo wa kukaushia mboga hizo  katika  katika maonyesho ya wakulima Nanene nane  mjini Morogoro Agosti 1, 2016. (Picha na Ofisi a waziri Mkuu)
NAN6 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizundua Banda la Maonyesho la wilaya ya  Temeke  kwenye maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agosti 1, 2016. Kushoto ni mkewe Mary. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN7Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizundua Banda la Maonyesho la wilaya ya  Temeke  kwenye maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agosti 1, 2016. Kulia kwake ni mkewe Mary  na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam , Paul Makonda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
NAN8 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama bidha mbalimbali  zinazotokana na zao la mronge zikiwema, dawa, mafuta na sabuni wakati alipoembelea meza ya Bibi Salome Kaiza   (kulia) kwenye banda la wilaya ya Tameke katika  maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro, Agosti, 1, 2016.  Kulia kwake ni Mkewe Mary. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN9Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama matikiti maji wakati walipotembelea meza ya Bwana Diocresty Theonesy kwenye banda la wilaya ya Temeke katika maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agost 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN11Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakipokezana  tikiti maji wakiwa kwenye meza ya Bwana  Diocresty Theonesy kwenye banda la Wilaya ya Temeke katika Maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agost 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NAN12 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakikagua mtama uliopandwa kwenye eneo la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro Agost 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Nibu Waziri Mh. Anastazia Wambura akagua eneo la ujenzi wa mageti ya kieletroniki katika Uwanja wa Taifa Leo

WU1Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura eneo eneo la ujenzi wa mageti ya kieletroniki katika Uwanja wa Taifa leo Agosti 1, 2016 Jijini Dar es Salaam.
WU2Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw.Julius Mgaya (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura na Katibu Mkuu Wizara ya hiyo Prof Elisante Ole Gabriel kuhusu ujenzi wa mageti ya kieletroniki katika Uwanja wa Taifa leo Agosti 1, 2016  Jijini Dar es Salaam.

Wanamichezo waaswa kutotumia dawa za kuongea nguvu katika michezo.

 Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.
Alex Nkenyenge akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanamichezo wanaokwenda
kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil  katika
mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 leo Agosti 1, 2016.
 Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice Tanzania Bw.
Maharage Chande  akishukuru Serikali kwa
fursa ya kuunga mkono jitihada za kuendeleza michezo wakati wa hafla ya kuwaaga
wanamichezo wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil  katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016
leo Agosti 1, 2016.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Prof Elisante Ole Gabriel akizungumza na wanamichezo na wadau wa
michezo  katika hafla ya kuwaaga
wanamichezo wanaoenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil  katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016
leo Agosti 1, 2016.
 Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.
 Anastazia Wambura akiongea na wanamichezo na wadau wa michezo  katika hafla ya kuwaaga wanamichezo wanaokwenda
kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil  katika
mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 leo Agosti 1, 2016.

Serikali yawashukuru wadau wa michezo kwa kushiriki katika maendeleo ya michezo nchini.

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akiongea na wanamichezo na wadau wa michezo  katika hafla ya kuwaaga wanamichezo wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil  katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 leo Agosti 1, 2016.
Picha/Habari na Raymond Mushumbusi
………………………………………………………………………………………………………….
Serikali imewashukuru wadau wa michezo nchini kwa kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kushiriki
na kudhamini michezo mbalimbali nchini.
Shukrani hizo zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa akizungumza na  wanamichezo wanaokwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 yanayofanyika Jijini Rio dejaneiro nchini Brazil.
Mhe. Anastazia Wambura amesema kuwa wadau wa michezo wamekuwa wakishirikiana na Serikali sio katika suala la michezo pekee hata katika habari na Sanaa na amewapongeza kampuni ya ving’amuzi ya Multichoice Tanzania (DSTV) na Bodi ya Utalii katika azma yao ya kuunga mkono maendeleo ya sera ya michezo nchini.
“Napenda kuwashukuru wadau wetu Dstv na Bodi ya Utalii, nawapongeza kwa kuona fursa hii muhimu na kuitumia kuwatia moyo wawakilishi wa nchi yetu katika michezo ya Olimpiki kwa mwaka 2016 mueendelee kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza sera ya maendeleo ya Michezo ili kufikia malengo” alisema Mhe. Anastazia.
Aidha amewataka wawakilishi wa Olimpiki kutumia fursa hii ya wadau wa michezo waliojitokeza kuwaunga mkono ikiwemo Bodi ya Utalii kutangaza utalii wa Tanzania kwa mataifa  mengine watakayo kutana nayo katika mashindano
ya Olimpiki nchini Brazil.
Kwa upande wake Mkurungezi Mkuu wa Multichoice Tanzania Bw.Maharage Chande ameishukuru Serikali kwa kuwapa fursa ya kushirikiana na timu ya Olimpiki kuitangaza michezo na kuitangaza Tanzania kimataifa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza michezo nchini.

Ilala yawataka wafanyabiashara kuzingatia muda wa usafi

DC ILALANa Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaaam imewataka wafanyabiashara kuzingatia muda uliopangwa na Serikali kwa ajili ya usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi unaofanywa kila ifikapo siku ya jumamosi.
Muda uliowekwa kwa ajili ya zoezi hilo ni kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi, ambapo wafanyabiashara wote watapaswa kufungua maduka na masoko yao mara baada ya zoezi hilo kukamilika.
Hayo yamesemwa leo na Afisa wa Manispaa hiyo, David Langa wakati alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii kuhusu mwitikio wa wananchi juu ya zoezi la usafi wa mazingira unaofanyika kila jumamosi na kila mwisho wa mwezi.
“Nawaomba Wafanyabiashara wenye tabia ya kujichelewesha ili wafike baada ya muda wa usafi pamoja na wale wanaofungua biashara kabla ya muda uliopangwa na Serikali kuacha mara moja kwani  lengo la kubadili muda wa kufungua biashara ni kwa ajili ya kufanya usafi” alisema Langa.
Akifafanua zaidi Langa aliwatahadharisha wananchi wanaopenda kutupa taka hovyo kuacha mara moja kwani sheria ya afya na sheria ya mazingira inapinga suala hilo na kwa mujibu wa sheria hizo adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka 6.
Kwa mujibu wa Langa alisema kuwa, suala la usafi sio suala la Serikali pekee bali wananchi wanatakiwa walifanye kuwa ni sehemu ya kulinda afya zao, hivyo kila mmoja anapaswa kuzingatia usafi kwenye maeneo yanayomzunguka.
Aidha Langa alisema kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzie kwani zoezi la kulipishwa faini bado ni endelevu, mtu atakaemkamata mwenzie anatupa taka atapewa shilingi elfu 20 na aliyekamatwa atatoa faini ya shilingi elfu 70.